NEWS

Monday, 24 February 2025

Nyambari Nyangwine achangia uzinduzi Filamu ya Himaya Nyakonga




Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine, amechangia shilingi milioni mbili taslimu katika uzinduzi wa Filamu ya Himaya ya Nyakonga ya kikundi cha waigizaji na waimbaji kilichopo wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Uzinduzi huo ulifanyika katani Nyakonga jana Februari 23, 2025, ambapo Nyambari aliungwa mkono na rafiki zake, hivyo kuwezesha shilingi milioni 3.8 kupatikana katika harambee hiyo ndogo.

Nyambari ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, aliwakilishwa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Magita katika uzinduzi wa filamu hiyo.

"Nyambari Nyangwine ni mtu mpenda maendeleo, sio mbinafsi. Uigizaji ni sanaa, ni kazi na ajira, niwatie shime wana-Nyakonga tusiione sanaa kama uhuni, sanaa ni ajira, sanaa ni fedha," alisema Magita.

Aliendelea: "Niwaombe vijana mshirikiane tutawasaidia, Nyambari ni mtu wa jamii ya wana-Tarime, anasaidia Tanzania nzima, sio hapa pekee."

Naye Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles alichangilia shilingi milioni 1.5, huku akikitia moyo kikundi hicho cha wasanii kuendelea kuibua vipaji.

Kiles ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, alimtaja Nyambari kama mpenda maendeleo aliyeamua kuwekeza kwenye elimu.



"Tutazidi kuwaombea, hata Rais wa Tanzania anawatambua wasanii mwendelee kuibua vipaji, siku moja mtakuwa kama wasanii wakubwa wanaonekana kwenye TV," Kiles alisema.

Kuhusu misaada ya kielimu, Kiles alisema "Sekondari zote Nyambari Nyangwine kazigusa kwa kupeleka vitabu, amewiwa kusaidia wananchi wa Tanzania kwenye elimu."

Kwa upande wake Mwenyekiti cha Filamu ya Himaya ya Nyakonga, Chacha Isaya Ryoba alimshukuru Nyambari kwa kuwapiga jeki na kutoa wito watu wengine kuiga mfano huo.

"Tunaimba na kuigiza, kilichotushawishi na kuanzisha filamu ni kukuza vipaji na kufika mbali, tunahitaji kuwa wasanii wakubwa hapa Tanzania, igizo linahamasisha maadili na jamii kuachana na mila na desturi potofu zinazokwamisha maendeleo ikiwemo elimu.

"Tunahamasisha jamii iwape watoto wa kike nafasi kuonesha vipaji vyao, sanaa ni kazi kama zingine, unaweza ukafanya ukajiingizia kipato," Ryoba alisema.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages