NEWS

Tuesday, 25 February 2025

Tarime: Mkuu wa Mkoa atoa maagizo mgogoro wa ardhi kata za Mwema na Regicheri



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi akitoa maagizo ya kupata msingi wa utatuzi wa mgogoro wa kugombea ardhi baina ya wakazi wa kata ya Mwema na Regicheri, wilayani Tarime jana Jumatatu.
----------------------------------

Na Christopher Gamaina, Tarime

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi ametoa maagizo matatu yanayolenga kupata suluhisho la kudumu la mgogoro wa miaka mingi wa kugombea ardhi baina ya wakazi wa kata za Mwema na Regicheri wilayani Tarime.

Kanali Mtambi ameagiza ufanyika utambuzi wa mpaka wa Inglam [uliowekwa na wakoloni], mpaka uliowekwa na serikali, sambamba na utambuzi wa wamiliki halali wa mashamba katika eneo linalogombewa.

Ameelekeza maagizo hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele na wataalamu wa ardhi kwa kushirikiana na wazee wa mila na wazee maarufu aliowateua kutoka pande zote mbili.


“Kazi ifanyike haraka iwezekanavyo kuanzia kesho (leo Jumanne) kisha nije kutoa maamuzi,” Kanali Mtambi aliagiza jana Jumatatu katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi na wananchi kutoka pande zote zinazozozana.

Aidha, kiongozi huyo wa mkoa aliwaonya wananchi wa pande zote kuepuka vitendo vya vurugu na kuharibiana mali kuanzia sasa.

“Ninataka mgogoro huu utatuliwe kwa amani na mtumie ardhi hii kulima mazao yanayakubalika,” Kanali Mtambi aliwambia wananchi hao.


Awali, wananchi wengi kutoka pande zote mbili waliopewa nafasi ya kutoa maoni yao juu ya mgogoro huo, waliishauri serikali kurejesha utambuzi wa mpaka wa Inglam ili kukata ‘mzizi wa fitina’.

Pia, walimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba kipande cha ardhi kinachogombewa ni ambacho kilivukwa wakati wa uwekeji wa vigingi vya mpaka unaotenganisha kata ya Mwema na Regicheri.

Mgogoro huo umekuwa ukisababisha wananchi wa pande hizo kupigana, kujeruhiana na kuuana kwa silaha za kijadi kama vile upinde, mishale na panga, sambamba na kuharibiana makazi yao na mazao ya chakula.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages