
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutosafirisha kahawa ghafi kwenda kuiuza nje ya bara hilo, badala yake ziwekeza kwenye viwanda vya usindikaji vya ndani ili kuongeza mapato na ajira katika nchi husika.
"Lazima tukubaliane hapa, kahawa inayozalishwa Afrika inapaswa kusindikwa hapa hapa Afrika na kisha iuzwe nje ya bara hili, kuendelea kusafirisha kahawa ghafi ni kuuza ajira ya vijana wa Afrika nje ya bara, kuua soko la kahawa na kuua mioyo ya wakulima kwani hawaoni manufaa ya kazi zao," amesema Rais Samia na kuendelea:
"Afrika inazalisha kahawa bora zaidi duniani, lakini bado tunabaki kuwa wauzaji wakuu wa kahawa ghafi. Tunapaswa kubadilisha hali hii kwa kuhakikisha kahawa inayozalishwa Afrika inaongezwa thamani hapa hapa katika bara la Afrika, na kuimarisha biashara ya kikanda, na ndipo iuzwe nje ya bara la Afrika."
Rais Samia alisisitiza hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa G25 wa Wakuu wa Nchi za Afrika zinazozalisha kahawa uliofanyika jijini Dar es salaam wiki iliyopita.
Alizihimiza nchi za Afrika na wadau wa sekta ya kahawa kuwekeza katika programu za mafunzo ya kilimo cha kisasa na pembejeo za kilimo kwa wakulima kama vile kuwapa miche, mbolea na dawa za kuua wadudu ili kuvutia vijana katika kilimo na usindikaji wa zao hilo la biashara.
Alisema kuna haja ya kuifanya Afrika kuwa soko kubwa la kahawa kwa kuhakikisha inalimwa kwa wingi na kusindikwa barani Afrika.
Kiongozi huyo wa nchi alisema serikali yake inaendelea na mkakati wa kutafuta masoko makubwa ya kahawa iliyosindikwa Tanzania kwa ajili ya mataifa mengine uakiwemo ya Mashariki ya Kati ambayo alisema ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa kahawa duniani.
Rais Samia alizisihi nchi za Afrika kukukubaliana kupitia Azimio la Dar es Salaam kuhusu kahwa, akisema linapaswa kuonesha njia ambayo zitatumia ili kuwa soko kubwa la kahawa Duniani.
Alisema Tanzania inalenga kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa, kwa kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo kwa kuwapa miche na ruzuku ya mbolea. “Kwa kufanya hivyo tutakuza soko la kahawa na kuvutia vijana,” alisisitiza.
Mkutano huo ambao ulikuwa na kaulimbiu isemayo "Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uendelezaji wa Sekta ya Kahawa Afrika", uliwaleta pamoja viongozi kutoka nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa, wataalamu wa sekta ya kahawa na wawekezaji ili kujadili njia za kufufua sekta ya kahawa barani Afrika.

No comments:
Post a Comment