NEWS

Tuesday, 29 April 2025

Elizabeth Msabi arejea kutoka UK, awa mwanamke wa kwanza kutangaza nia ya ubunge Tarime Vijijini kupitia CCM



Elizabeth Thomas Msabi akizunguma na Mara Online News mjini Tarime jana Jumatatu.
-----------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Tarime

Katika tukio la kihistoria, Elizabeth Thomas Msabi, Mtanzania aliyeishi Uingereza (UK) kwa miaka takriban 20, amerejea nchini kwake na kuwa mwanamke wa kwanza kutangaza nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Tarime Vijijini katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia chama tawala - CCM.

Kwa furaha na msisitizo mkubwa, Elizabeth mwenye umri wa miaka 46, anasema amewiwa kurejea kutoka ughaibuni akiwa na shauku kubwa ya kuleta kwenye jimbo lake la asili maarifa aliyovuna huko, kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Elizabeth, ambaye alihamia Uingereza kwa ajili ya masomo na baadaye kufanya kazi katika sekta mbalimbali za maendeleo na usimamizi wa miradi ya kijamii, anasisitiza kuwa amerudi nyumbani kwa dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya yanayokidhi mahitaji ya wananchi wa Tarime Vijijini.

Akiwa na elimu ya chuo kikuu kuhusu masuala ya afya na kusaidia watu wenye uhitaji, wakiwemo watoto, wanawake na wazee, Elizabeth anasema sasa ni wakati wake wa kuwekeza maarifa hayo katika ustawi wa jamii iliyomlea, kwani ana uzoefu mpana wa kimataifa.

“Nimepata fursa ya kujifunza mengi nje ya nchi – sasa ni wakati wa kurudisha kile nilichojifunza kwa jamii yangu,” Elizabeth ambaye pia aliwahi kuwa Sista wa Kanisa Katoliki alisema kwa msisitizo katika mahojiano maalum na Mara Online News mjini Tarime jana Jumatatu.

Anasema anaona fahari ya kuwa na maono makubwa ya kuleta mapinduzi chanya, hasa katika sekta za afya na elimu, pamoja na kukuza fursa za kiuchumi kwa manufaa mapana ya wananchi wa Tarime Vijijini.

Elizabeth pia anaamini kwamba maendeleo ya kweli huanzia chini, na kwamba kwa kushirikiana na wananchi, anaweza kusaidia kulibadilisha jimbo la Tarime Vijijini, mkoani Mara kuwa kitovu cha maendeleo endelevu ya kisekta.

Kwa macho ya wengi, Elizabeth Thomas Msabi si tu mgombea wa kisiasa, bali pia ni mfano wa kuigwa kwa Watanzania walioko nje ya nchi – akionesha kuwa bado wana nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii yao ya asili.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages