
Muonekano wa sehemu ya mbele ya CMG Hotels Ltd
Na Mwandishi Maalumu
Mei 3, 2025, itakuwa siku ya kihistoria kwa mji wa Tarime, mkoani Mara, baada ya uzinduzi rasmi wa Hoteli ya kifahari ya CMG - iliyofanyiwa maboresho makubwa kwa viwango vya kuvutia kila mgeni atakayeitembelea.
Maboresho hayo yameifanya hoteli hii kuwa sehemu bora zaidi kwa malazi, chakula na burudani, lakini pia kivutio kipya cha utalii na kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi katika mji huo.
Kwa hadhi ya huduma zake za kimataifa, CMG Hotels Ltd itakuwa kivutio cha aina yake, ikilinganishwa na miji ya kifahari duniani kama Dubai.
Wateja watafurahia huduma zenye hadhi ya kimataifa kama vile vyumba vya kulala vyenye mandhari ya kuvutia, vyakula vya kila aina, kumbi bora za mikutano na “swimming pools” za kisasa, miongoni mwa burudani nyingine.
Ubora wa hoteli hii utaiweka Tarime kwenye ramani ya kimataifa kama kituo kipya cha utalii wa kifahari nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
CMG Hotels Ltd ipo kilomita chache kutoka mpaka wa Tanzania na Kenya, pamoja na hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti, hali inayoiweka hoteli hii katika nafasi ya kipekee ya kuvutia wageni wa kimataifa na wa ndani.
Watalii wanaoingia kupitia mpaka wa Sirari na wanaotembelea Hifadhi ya Serengeti sasa watakuwa na sehemu nzuri ya kupumzika, kula, kunywa na kupata huduma nyingine bora zaidi.
“Tumeboresha sana vyumba vya kulala kwa viwango vya kimataifa. Ukiingia kwenye chumba cha hoteli ya kifahari kule Dubai ukafumba macho, kisha ukaja ukaingizwa kwenye chumba cha hapa CMG na kufumbua macho, utafikiri bado uko Dubai.
“Tumeboresha pia vyumba vya suti ambavyo kiongozi yeyote wa nchi hata rais anaweza akakaa na wasaidizi wake,” anasema Mkurugenzi wa CMG Hotels Ltd, Christopher Mwita Gachuma.
Maboresho ya hoteli hii yamehusisha pia ujenzi wa baa ya nje, jiko kubwa la kuchuma choma, vibanda vya kupumzika, vyumba vya sauna, mazoezi (gym) na huduma za massage.
“Pia, tumetenga maeneo maalum kwa ajili ya wageni kujenga mahema yao, kupiga picha na michezo ya watoto,” Gachuma aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara hotelini hapo wiki iliyopita
Mkurugenzi wa CMG Hotels Ltd, Christopher Mwita Gachuma.Kuhusu watoa huduma, Gachuma anasema wamemeajiri wafanyakazi takriban 60, wakiwemo wapishi wa kimataifa kutoka kwenye hoteli za kifahari jijini Dar es Salaam, wenye taaluma ya kupika kila aina ya vyakula, vikiwemo vya Kichina, Kihindi, Kiafrika na Kizungu.
“Tumealika viongozi, marafiki na wateja watakaohudhuria hafla ya uzinduzi wa hoteli yetu, na kwa upande wa burudani, mwanamuziki Diamond Platnumz ameshathibitisha kuja, lakini pia na wasanii wengine watakuwepo,” anasema Gachuma ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.
Hoteli hii ya CMG inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tarime na maeneo ya jirani. Mfano, Halmashauri ya Mji wa Tarime itakusanya mapato zaidi kupitia ushuru wa huduma, kodi na shughuli za kibiashara zitakazochipuka kutokana na ongezeko la wageni.
Aidha, kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kutaongeza fursa za ajira kwa wakazi wa mji wa Tarime katika sekta nyingi kama vile utalii, usafirishaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali.
Fursa kwa wakulima, wafugaji
Wakulima na wafugaji katika mji wa Tarime na wilaya jirani wanatarajiwa kunufaika zaidi kutokana na mahitaji mapya ya bidhaa za chakula, matunda, maziwa, nyama, mayai na nyinginezo zinazohitajika katika hoteli hii ya CMG.
Soko hili jipya na kubwa litaongeza kipato cha wakulima na wafugaji, na hivyo kuchangia kuboresha maisha ya wananchi katika mji wa Tarime.
Gachuma anasema lengo la kufanya uwekezaji mkubwa wa hoteli hii ni kukuza utalii na kuinua uchumi katika mji wa Tarime ambao pia una uwanja mdogo wa ndege katika eneo la Magena.
“Kutokana na uwepo wa hoteli hii, Uwanja wa Ndege Magena utatumiwa sana na watalii - watashukia pale na kuja kupumzika hapa na kufanya maandalizi ya kwenda mbugani [Hifadhi ya Taifa Serengeti],” anasema mkurugenzi huyo wa CMG Hotels Ltd.
Anaendelea: “Tunaona sasa hivi barabara ya kwenda Serengeti inawekwa lami, kwa hiyo hoteli hii itakuwa kituo kimojawapo cha kuchochea utalii katika ukanda huu.”
DC Gowele ampa kongole
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele, anamshukuru Gachuma kwa kuiheshimisha wilaya hiyo kwa uwekezaji huo mkubwa.
“Tunamshukuru sana Mkurugenzi Gachuma kwa kuleta Dubai Tarime. Hoteli hii ni kivutio kikubwa cha utalii katika wilaya yetu, itaongeza hadhi ya mji wetu na kuongeza mapato ya halmashauri yetu,” anasema Meja Gowele.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele.
Meja Gowele alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi wa Tarime, vikiwemo vikundi vya vijana na wanawake vinavyopata mikopo ya mitaji kutoka Halmashauri ya Mji kutumia fursa ya uwepo wa hoteli hiyo kujikwamua kiuchumi.
Anashauri vikundi hivyo kuchangamkia fursa hiyo kwa kuzalisha mazao ya kilimo na mifugo kama vile matunda, mboga mboga, kuku na mayai kwa ajili ya kuuza kwenye Hoteli ya CMG. ”Hili ni soko jipya na kubwa,” anasisitiza.
Kwa mujibu wa Meja Gowele, kuzinduliwa kwa hoteli hii ya kifahati kumeipa serikali msukumo mpya wa kuendelea kuboresha Uwanja wa Ndege Magena, kwani watalii sasa wamepata sehemu bora ya kupumzika.
Kwa ujumla, uzinduzi wa CMG Hotels Ltd utafungua ukurasa mpya utakaoufanya mji wa Tarime kufahamika kimataifa, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa maisha ya wakazi wake na kuifanya Tarime kuwa "Dubai ndogo" ya Tanzania na Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment