
Jaji George Mcheche Masaju
Na Mwandishi Wetu
Jaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, George Mcheche Masaju, anatarajiwa kuapishwa kesho Jumapili Juni 15, 2025 jijini Dodoma.
Jaji Masaju aliteuliwa jana Ijumaa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuchukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye amestaafu.
Kiongozi huyo wa mhimili wa tatu wa dola alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli (hayati).
Masaju anakuwa Jaji Mkuu wa tisa tangu uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961.
Majaji wengine waliowahi kuhudumu katika nafasi hiyo baada ya uhuru ni Ralph Windham, Philip Telford Georges, Augustine Saidi, Francis Lucas Nyalali, Barnabas Samatta, Augustine Ramadhani, Mohamed Chande Othman na Ibrahim Hamis Juma.
Nafasi ya Jaji Mkuu ni cheo cha juu katika mfumo wa mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo mtu anayeshika nafasi hiyo anateuliwa na Rais kuwa kiongozi wa Mahakama ya Juu ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano.
Tangu uhuru kutoka kwa Waingereza, Mahakama ya Tanzania imepitia marekebisho mbalimbali ya sheria ili zifanane na mazingira yaliyopo, hasa kwa kuzingatia kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
No comments:
Post a Comment