
Diwani wa Kata ya Nyakonga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles "K", akihutubia mkutano wa hadhara katani humo jana Juni 11, 2025.
---------------------------------------
Na Godfrey Marwa, Tarime
Diwani wa Kata ya Nyakonga katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, Simion Kiles “K”, amesema wananchi wa kata hiyo wana kila sababu ya kujivunia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025.
Kiles ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara katani hapo jana, ambapo aliwasomea wananchi utekelezaji wa ilani hiyo.

Wananchi wakimshangilia Diwani Kiles (hayupo pichani) wakati akihutubia mkutano wa hadhara katani Nyakonga jana.
----------------------------------------

Kwa mujibu wa Kiles, katika kipindi cha mwaka 2020-2025, shilingi bilioni tatu zimetumika kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali katani Nyakonga, ikiwemo ya elimu, afya, maji, barabara, umeme na kuanzisha vikundi vya maendeleo ya jamii.
Kiongozi huyo alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni 139.7 ni michango ya wananchi, shilingi milioni 154.6 ni mchango kutoka mfuko wake binafsi na kiasi kilichobaki kilitokana na mapato ya ndani na Serikali Kuu.
"Tuungane tuwe wamoja kwenye maendeleo, siasa ni vitu vya kupita, tujenge Nyakonga yetu. Kama kuna mgombea wako mwambie tusitengenezeane ajali,” alisema Kiles na kuendelea:
"Tunahitaji watia nia wengi kupata ushindani, anayesema hakuna kilichofanyika maana yake mpaka ninyi hamjafanya kitu, Rais, mbunge na diwani hawajafanya kitu. Sasa hivi tunao wimbo mmoja pekee - mitano tena kwa Mama Samia, Mwinyi na Dkt. Nchimbi."
Wakati huo huo, jumuia zote za CCM katika kata ya Nyakonga zilimtunuku Diwani Kiles tuzo mbalimbali kwa kutambua mchango wake wa hali na mali katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho tawala.

Mwakilishi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Nyakonga akimkabidhi Diwani Kiles (kushoto) cheti cha pongezi.
--------------------------------------------
Katika hatua nyingine, Kiles alikabidhi msaada wa pikipiki mpya kwa Kikundi cha Vijana cha Ufugaji Samaki na Kilimo Kebweye - iliyotolewa na Nyambari Nyangwine aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010 hadi 2015.
Nyangwine ametoa msaada huo kama sehemu ya kuunga juhudi za Diwani Kiles katika kuwasaidia vijana wa kata ya Nyakonga kujikwamua kiuchumi.
Awali, Kiles alitembelea ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi katika Shule ya Msingi Kebweye na kutoa shilingi milioni nne kuchangia ujenzi huo.
Baadaye diwani huyo alitembelea vijiwe mbalimbali vya wajasiriamali katani humo, wakiwemo akinamama wanaouza mbogamboga na kuwashika mkono kwa fedha taslimu na miavuli, huku akiwahimiza kujiunga katika vikundi kwa ajili ya kujiletea maendeleo kwa haraka.


Picha zote na Mara Online News
No comments:
Post a Comment