
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Mining Corporation, Mark Bristow, akishirikiana na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, kukabidhi hundi ya msaada wa shilingi milioni 20 kwa viongozi wa taasisi ya St. Justin Foundation ya mkoani Mara wakari wa hafla iliyofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu juzi.
------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Taasisi ya kimataifa ya Nos Vies en Partage (NVeP), kwa kushirikiana na kampuni ya Barrick, imetoa msaada wa shilingi milioni 80 kwa mashirika manne yasiyo ya kiserikali kutoka mikoa ya Shinyanga, Mara, Dodoma na Pwani kwa ajili ya kukabilianana changamoto mbalimbali za kijamii.
Mashirika yaliyonufaika na msaada huo kila moja ikiwa imepata shilingi milioni 20 ni Busindi Asali, St. Justin Foundation, Nazareti Group-Nkulabi na Sustainable Planet Foundation.
Msaada huo umetokana na sehemu ya fedha zilizotolewa na taasisi ya NVeP iliyoanzishwa na inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick Mining Corporation, Mark Bristow, kwa ajili ya kusaidia makundi maalum kama vile wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji yasiofaidika na ukuaji wa kiuchumi barani Afrika.
Kila robo ya mwaka, NVeP hutoa misaada yenye tija na manufaa ya moja kwa moja kwenye jamii mbalimbali zenye uhitaji barani Afrika, ambapo kufikia sasa zaidi mashirika zaidi ya 35 yasiyo ya kiserikali na taasisi za kijamii nchini Tanzania yamepatiwa msaada huo, na tayari umeleta mabadiliko chanya katika jamii, hususan katika sekta za elimu, afya kwa wanawake na watoto, utunzaji wa mazingira na kuendeleza miradi midogo midogo ya kujikwamua kimaisha.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada wakati wa ziara yake ya kikazi iliyofanyika kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga juzi, Bristow alisema NVeP itaendelea kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi ambazo zinazohudumia jamii kuendana na malengo ya taasisi hiyo, sambamba na kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Meneja wa taasisi ya St. Justin Foundation yenye makao mkoani Mara, Juma Songo, akizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzake, aliishukuru NVeP kwa msaada huo, akisema utaisaidia kukabiliana na changamoto za kijamii.
Naye Katibu wa Kikundi cha Busindi Asali, Tatu Lukuba, alisema msaada huo kwao ni mkubwa na utawawezesha kupanua mradi wao wa ufugaji wa nyuki na kuwezesha wanakikundi kujikwamua kimaisha na kuboresha maisha yao na familia zao.
“Waswahili walisema akufaaye kwa dhiki ni rafiki, tunashukuru msaada huu mkubwa tulioupata kutoka NVeP na Barrick,” alisema Lukuba.
No comments:
Post a Comment