NEWS

Saturday 28 November 2020

Wasichana waliokimbilia ATFGM Masanga waendelea kuhitimu masomo ya sekondari

Wanafunzi wanaosomeshwa na Shirika la ATFGM Masanga katika Shule ya Sekondari ya Central Buhongwa jijini Mwanza.

 

WASICHANA saba waliokimbilia kituo okozi cha ATFGM Masanga kukwepa shinikizo la kukeketwa na kuolewa kutoka kwa wazazi wao, ni miongoni mwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Central Buhonjwa ya jijini Mwanza.

 

Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani, pia mvulana aliyepelekwa na kituo hicho kusoma shuleni hapo anahitimu kidato cha nne, huku wengine wanne (wasichana wawili na wavulana wawili) wakibaki kuendelea na masomo ya kidato cha pili (mmoja) na cha tatu (watatu).

 

“Hawa wasichana ni miongoni mwa wengi waliokimbilia kituoni kwetu wakiwa wamefukuzwa na wazazi wao kwenye familiza zao baada ya kukataa mashinikizo ya kukeketwa na kuolewa.

 

“Watoto wa kiume wanaokimbilia kituoni kwetu ni ambao wamefukuzwa na wazazi wao baada ya kukataa kwenda kutahiriwa kwa mara ya pili kienyeji huku wakiwa tayari wameshafanyiwa tohara ya kisasa hospitalini.

 

“Kwa ujumba watoto wanaokataa mila na desturi hizo wanakataliwa, wanafukuzwa na wazazi nyumbani na wanakosa kabisa fursa ya kwenda shule,” amesema Mgani katika mazungumzo na Mara Online News, hivi karibuni.

 

Amesema idadi kubwa ya wasichana na wavulana wanaofukuzwa na wazazi wao baada ya kukataa kutekeleza mila hizo ni kutoka wilaya ya Tarime, hasa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime – ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara.

 

“Lakini pia wapo wanaotoka wilaya za Butiama na Serengeti mkoani Mara na nchi jirani ya Kenya,” ameongeza Meneja Mradi huyo wa ATFGM Masanga.

 

Amesema shirika hilo lisilo la kiserikali linawapokea na kuwasaidia watoto wa aina hiyo katika mahitaji ya malazi, chakula, mavazi, matibabu na masomo - kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.

 

Watoto wanaopokewa katika kituo hicho, kwa mujibu wa Mgani, ni wenye umri wa miaka kati ya minane na 17 waliofukuzwa na wazazi wao baada ya kukataa kukeketwa, kutahiriwa kienyeji, kuolewa na kuoa.

 

“Tunawasaidia watoto hawa wakati huo huo tunaendelea kufanya majadiliano na wazazi wao kuona namna ya kuweza kuwarudisha kwenye familia zao,” amesema na kuendelea:

 

“Mwaka jana [2019] tulikuwa na watoto 557 lakini baadaye tulibaki na 77, hivyo utaona kwamba baada ya usuluhishi - watoto zaidi ya 400 wamepokewa na wazazi wao.”

 

Mgani amesema kwamba kwa sasa Shirika la ATFGM Masanga kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, linalea watoto wa kike 115 kituoni wenye umri wa miaka kati ya minane na 17.

 

Aidha, amesema shirika hilo limeshaokoa watoto zaidi ya 400, wengi wao wakiwa wasichana tangu mwaka 2008 lilipoanzisha kambi okozi ya kunusuru wasichana wanaokuwa katika hatari ya kukeketwa na kuozwa.

Meneja Mradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani akiwa na wanafunzi wanaosomeshwa na shirika hilo katika Shule ya Sekondari ya Central Buhongwa.


Mgani amefafanua kuwa watoto hao wamewezeshwa kupata elimu ya msingi hadi kidato cha sita, vyuo vya mafunzo ya ujasiriamali na ufundi mbalimbali na vyuo vikuu - kwa ufadhili wa Shirika la Terre des Hommes la Uholanzi.

 

Mbali ya Terre des Hommes, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) limekuwa likifadhili ATFGM Masanga kupambana na vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni.

 

“Lakini kuna watoto wanaoendelea kusoma vyuoni, pia wapo ambao tayari wamepata kazi baada ya kumaliza masomo vyuoni na wengine wanatafuta ajira,” amefafanua Mgani.

Wanafunzi wanaosomeshwa na Shirika la ATFGM Masanga.

 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na ATFGM Masanga, mila za ukeketaji na kuoza watoto katika umri mdogo zinachangiwa na umaskini uliokithiri miongoni mwa jamii husika.

 

“Unakuta kuna watu wanategemea ukeketaji kujipatia kipato, lakini pia wazazi wanalazimisha mtoto akeketwe ili aolewe na kuwapatia ng’ombe, vilevile wengi hawana elimu juu ya madhara ya mila hizo,” amesema Mgani.

 

Meneja Mradi huyo wa ATFGM Masanga ametaja madhara ya vitendo vya ukeketaji na ndoa katika umri mdogo kuwa ni pamoja na kuwakosesha watoto fursa ya kusoma, ufaulu duni katika masomo na kuwaathiri kiafya na kisaikolojia.

 

Kutokana na hali hiyo, Mgani ametoa wito kwa wazazi na jamii husika kwa ujumla kubadilika ili kuwaepushia watoto madhara hayo, vinginevyo watajikuta wanaishia kwenye mikono ya dola kwa kukaidi sheria za nchi na kimataifa zinazokataza vitendo hivyo vya ukatili na unyanyasaji watoto kijinsia.

 

(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages