NEWS

Sunday 29 November 2020

Wakulima eneo oevu la Mara wahofia mafuriko tena

Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji ukanda wa Mara Kaskazini, Siproza Charles (kushoto) na wakulima wenzake wakionesha sehemu ya mashamba yao katika eneo oevu jirani na mto Mara.


WAKULIMA katika eneo oevu la mto Mara nchini Tanzania wameanza kupanda mazao ya chakula huku wakihofia yanaweza kusombwa na mafuriko tena.

 

Aprili na Mei mwaka huu, mafuriko yalisomba mazao mbalimbali katika mashamba vijiji vilivyopo jirani na mto huo na kuwaacha wakulima bila mavuno.

 

“Msimu uliopita maji yalijaa katika haya mashamba na sikuvuna chochote. Nimeanza kupanda tena kujaribu,” Goryo Marwa ameiambia Mara Online News kijijini Mara-Sibora, hivi karibuni.

 

Mara-Sibora ni mojawapo wa vijiji vilivyopo kandokando ya mto Mara ambapo wakazi wake hutegemea kilimo cha mazao ya chakula kama mahindi na mihogo yanayolimwa katika eneo oevu la mto huo.

Wakulima na wakazi wa kijiji cha Mara-Sibora, Akuti Atieno (kulia) na Goryo Marwa, wakizungumza na Mara Online News katika eneo oevu la mto Mara ambako wamekuwa wakilima mazao mbalimbali.


 

“Hatuna sehemu nyingine ya kulima, tunategemea hapa na ndio maana tunalazimika kujaribu tena hata kama mvua zimeanza kunyesha,” amesema Marwa ambaye ameanza kupanda mahindi katika mashamba yake.

 

Baadhi ya wakulima wanalima na kupanda mazao katika maeneo hayo wakiwa na hofu kutokana na mafuriko Aprili na Mei, mwaka huu.

 

“Maji yalichukua ekari tano za mashamba yangu, nikabaki katika shida ya kununua chakula. Kwa sasa nimeogopa kupanda mazao kwenye eneo lote, nimepanda sehemu kidogo kwa sababu naogopa maji yanaweza kujaa tena na kusoma kila kitu,” amesema Akuti Atieno ambaye pia ni mkulima katika eneo oevu la mto Mara lililokumbwa na mafuriko.

 

Wakulima wanasema eneo oevu la mto Mata lina ardhi yenye rotuba ya asili inayostawisha mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, mihogo na mbogamboga.

 

“Eneo hili ndilo wakulima wanategemea kupanda mazao ya chakula na biashara, hawana njia nyingine na hawahitaji mbolea, mazao yanastawi sana,” amesema Siproza Charles ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji ukanda wa Mara Kaskazini.

 

Hata hivyo, Siproza amesema wakulima wa maeneo hayo wameanza kuchukua tahadhari baada ya mafuriko kusomba mashamba yao katika msimu uliopita.

 

“Msimu uliopita mazao yote yalisombwa katika mashamba yaliyopo eneo oevu na kwa sasa wakulima wanapanda kwa tahadhari,” amesema Siproza.

Mkulima na mkazi wa kijiji cha Mara-Sibora, Sproza Charles akiponesha sehemu ya shamba lake katika eneo oevu la mto Mara.

 

Inakadiriwa kuwa zaidi ya kaya 400 ziliathiriwa na mafuriko katika kijiji cha Mara-SIbora pekee katika msimu wa kilimo uliopita, kwa mujibu wa Siproza.

 

Baadhi ya vijiji vyenye wakulima walioathirika na mafuriko ya Aprili na Mei mwaka huu ni Matongo, Kerende, Nyabichune, Bisarwi na Weigita.

 

Hali ilikuwa mbaya zaidi katika kijiji cha Matongo ambako mbali na mashamba, maji yalizingira mazizi ya mifugo na baadhi ya kaya zilihamishwa kwa msaada kutoka mgodi wa dhahabu wa North Mara.

 

“Ilifikia hatua watu wakapanda kwenye miti kunusuri maisha yao,” amesema Mwita Seri ambaye ni katibu wa watumia maji ukanda wa Tigithe Chini uliopo ndani ya bonde la mto Mara.

 

Mafuriko hayo yalitokea katika kipindi ambacho mlipuko wa virusi vya Corona ulikuwa imeripotiwa katika baadhi ya nchi za Afrika, lakini Siproza anasema janga hilo halikuwa na madhara yoyote kwa wananchi wanaoishi kandokando ya mto Mara.

 

“Sisi Corona tuliisikia tu, hatukuwahi kuwa na mgonjwa au kuona mgonjwa wa Corona,” amesema Siproza.

 

Kwa mujibu wa Siproza, mafuriko hayo yalivunja rekodi na kuleta taharuki kwa wakulima, wafugaji na wachimbaji wadogo wa madini.

 

“Mwaka 1977 mafuriko yalitokea lakini sio kama hayo, kipindi hiki yalitisha,” amesema Siproza ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa serikali ya kijiji.

Mojawapo ya mashamba yaliyoandaliwa kwa ajili ya kupanda mazao katika eneo oevu la mto Mara.

 

Kilichotokea kwa wachimbaji wadogo

 

Mafuriko hayo ya Aprili na Mei, hayakuwaacha salama wachimbaji wadogo wa madini wanaoishi jirani na mto Mara.

 

“Mafuriko ya maji yalijaa kwenye mashimo na kusomba mchanga wa dhahabu,” amesema Seri ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa jukwaa la dakio la Mara-Mori.

 

Kilichosababisha mafuriko

 

Wataalamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) wanasema mafuriko hayo yalisababishwa na mvua nyingi zilizonyesha kwa miezi kadhaa mfululizo na kujaza maji mto Mara na katika maeneo ya nje ya mto.

Mmoja wa wakulima walioathiriwa na mafuriko katika shughuli za kilimo, Sproza Charles, akizungumza na Mara Online News kwenye eneo oevu la mto Mara ambako wamekuwa wakilima mazao mbalimbali.

 

“Mvua zilikuwa nyingi, na sio tu mto Mara uliojaa maji bali hata Ziwa Victoria yalivunja rekodi,” amesema Wiston Agwaro ambaye ni mhaidrojia wa LVBWB ofisi za Musoma mkoani Mara.

 

Agwaro amesema mafurio hayo yalisomba mazao na mifugo akitaja vijiji vingine vilivyoathirika zaidi kuwa ni Buswahili kilichopo wilayani Butiama na Wegero (Musoma).

 

Suluhisho

 

Mhaidrojia Agwaro amesema mafuriko hayawezi kuzuilika na yanakuja kama majanga mengine, hivyo kinachotakiwa ni wananchi kuchukua tahadhari.

 

“Mafuriko ni janga la asili, suluhisho ni watu kuacha shughuli za kilimo na makazi katika maeneo oevu kando kando ya mto Mara,” ameshauri mtaalaamu huyo wa kutoka LVBWB.

 

(Imeandikwa na Mugini Jacob, Mara)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages