Wafanyakazi wa MFEC, walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kewamamba katika hafla ya kukabidhi msaada wa vyombo vya upishi na kunywea uji shuleni hapo. |
SHULE ya Msingi Kewamamba katika wilaya ya Tarime mkoani Mara imepokea msaada wa vyombo mbalimbali vya upishi na kunywea uji kutoka Kituo cha Maendeleo ya Kilimo Mogabiri (MFEC).
Akikabidhi vifaa hivyo jana Jumanne Desemba 8, 2020, Meneja wa MFEC, Roselyne Mosama amesema wametoa msaada huo kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni.
Wafanyakazi wa MFEC wakiandaa msaada wa vyombo vya upishi na kunywea uji katika Shule ya Msingi Kewabamba. |
Meneja wa MFEC, Roselyne Mosama (kushoto) akikabidhi mwanafunzi vikombe vya kunywea uji katika Shule ya Msingi Kewamamba. |
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na sufuria, ndoo, majagi, vikombe na miiko kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi wa shule hiyo kuanza kunywa uji kutokana na mashamba darasa yatakayoandaliwa katika maeneo ya shule hiyo kwa kushirikiano wa MFEC na maafisa ugani wa kata ya Kiore.
Meneja wa MFEC, Roselyne Mosama (kushoto) akiendela kukabidhi vyombo hivyo kwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Kewamamba. |
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kewamamba (kulia) akipokea msaada wa sufuria kutoka kwa mfanyakazi wa MFEC katika hafla hiyo. |
Tayari yamefanyika maadalizi ya uanzishaji wa mashamba darasa ya mahindi, maharage, viazi vitamu na migomba shuleni hapo; mazao ambayo yatatumika kwa ajili ya chakula cha wanafunzi.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kewamamba wakishangilia wakati wa hafla ya makabidhiano hayo ya vyombo vya upishi na kunywea uji shuleni hapo. |
Mosama amefafanua kuwa walianza kutekeleza mpango huo mwaka 2017, na kwamba Shule ya Msingi Kewamambo imekuwa ya pili kupata msaada huo baada ya ile ya Abainano.
“Tuna utaratibu wa kutoa msaada kila siku ya Jumanne ya kwanza ya Desemba kila mwaka,” amesema Meneja huyo wa MFEC akifafanua kuwa siku hiyo inajulikana kwa jina la Giving Tuesday.
Mwaka jana, kwa mubibu wa Mosama, MFEC ilipeleka msaada wa mashuka katika kituo cha afya Magoto kwa ajili ya wagonjwa.
Ameongeza kuwa kituo hicho kimewiwa kutoa misaada ya aina hiyo baada ya kubaini kwamba familia nyingi hazina uwezo wa kumudu mahitaji ya chakula kwa watoto wao wanapokuwa shuleni.
Meneja wa MFEC, Roselyne Mosama (aliyesimama) akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi msaada wa vyombo vya upishi na kunywea uji katika Shule ya Msingi Kewamamba. |
“Mtoto anapokosa chakula inamwia vigumu kuzingatia masomo… wakifeli mtihani wa darasa la saba tunawalaumu. Mtoto kama hujashiba, hujalala vizuri hawezi kusoma vizuri. Lakini kama mtoto anapata lishe bora atasoma vizuri na atafaulu vizuri, vinginevyo labda awe na tatizo kubwa sana,” amesema Mosama.
Hali ilivyokuwa kabla ya kukabidhi vyombo hivyo. |
Walimu wa shule hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewamamba na Diwani wa Kata ya Kiore, Rhobi John ambaye alicha kazi ya ukeketaji baada ya kuelimishwa na MFEC, wamewataka wazazi kuunga mkono hatua hiyo iliyoanzishwa na Kituo hicho ili kuwezesha wanafunzi kupata chakula shuleni.
Meneja wa MFEC, Roselyne Mosama akizungumza katika hafla hiyo. |
Mkazi wa kijiji hicho, Kennedy Mniko ameishukuru MFEC kwa msaada huo akisema utachochea ari ya wanafunzi kusoma kwa bidii na kuinua kiwango cha taaluma yao.
“Sisi kama wazazi tunawashukuru MFEC kwa kuiona changamoto hii na kuanzisha mpango huu wa kusaidia watoto wetu kuanza kupata angalau uji wakiwa shuleni. Ni kweli watoto wetu wamekuwa hawafanyi vizuri katika mitihani kutokana na njaa. Wazazi tuko tayari kuunga mkono hatua hii ya MFEC ili watoto wetu waendelee kupata huduma hii na kufurahia masomo,” amesema Mniko.
(Habari na picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment