NEWS

Friday 11 December 2020

Makuruma rasmi uenyekiti wa halmashauri Serengeti, Mbunge, DC wanena

Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Makuruma akihutubia madiwani.


BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara limemchagua Diwani wa Kata ya Busawe, Ayub Makuruma kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

 

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Desemba 11, 2020 kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo baada ya madiwani wateule 40 kula viapo vya utumishi na maadili, Makuruma ambaye hakuwa na mshindani katika kinyang’anyiro hicho, amepigiwa kura zote 41 za ndiyo ikiwemo ya Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi.

 

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo imechukuliwa na Diwani wa Kata ya Kisangura, Samson Wambura ambaye naye amepigiwa kura zote 41 za ndiyo.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti akiwemo Jackline Mwita (katikati) wakila kiapo cha utumishi na maadili.

 

Akizungumza baada ya kuchaguliwa na kuunda kamati za madiwani, Makuruma amewashukuru madiwani kwa ushindi huo na kuwaahidi ushirikiano wa hali ya juu katika kushughulikia maendeleo ya wana-Serengeti.

 

“Siasa imeisha twendeni tukachape kazi za kuwaletea wananchi maendeleo. Nitatenda haki na kusimamia usawa, ninawaahidi maximum corporation (ushirikiano wa hali ya juu),” Makuruma amewaambia madiwani.

 

Amesisitiza kuwa madiwani wana jukumu kubwa la kuhamasisha na kusimamia uboreshaji wa huduma za kijamii ikiwemo kuhakikisha barabara za vijijini na maeneo mengine zinapitika kirahisi wakati wote.

Madiwani wakiendelea kula kiapo. Wa kwanza kushoto ni Diwani wa Kata ya Ikoma, Michael Kunani.


Makuruma ametumia nafasi hiyo pia kuwataka madiwani wote kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wakiwemo Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Mkurugenzi wa Halmashauri katika kuwaondolea wananchi vikwazo vya maendeleo.

 

Aidha, Mwenyekiti huyo wa halmashauri ameahidi kushirikiana na viongozi wengine kuhakikisha madiwani hao wanapata fursa za kufanya ziara za mafunzo mbalimbali nje ya Serengeti.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Serengeti, Mhandisi Juma Hamsini (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho.

 

Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho.

 

Naye Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi, ametumia nafasi hiyo kutangaza vipaumbele vyake vitano vya kuharakisha maendeleo ya wilaya ya Serengeti.

 

Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni elimu na afya, utawala bora, mazingira na utalii, uchumi na miundombinu inayohusisha ujenzi wa miji na uwanja wa ndege wa Mugumu.

 

“Tukishirikiana tunaweza kuifanya Serengeti kuwa vile tunataka iwe,” amesema mbunge huyo.

 

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, amewataka madiwani wote kwenda kuhamasisha na kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari kwenye maeneo yao ya uongozi ili kuwezesha wanafunzi wote watakaoripoti mwakani kusoma bila msongamano.

 

“Watoto ni wetu, kwa hiyo lazima tujenge madarasa wasome, vinginevyo tuache kuzaa. Kwa sasa tunahitaji vyumba vya madarasa 147 katika shule za msingi na sekondari wilayani,” amesema Babu.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages