NEWS

Thursday 17 December 2020

Sababu ya wanyamapori Serengeti kupenda kunywa maji ya mto Mara

Nyumbu wa Serengeti wakivuka mto Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

HUWEZI kuzungumzia uhifadhi na umaarufu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) bila kutaja mto Mara. Hii ni kutokana na mto huo kuwa tegemeo muhimu la maji na makazi kwa wanyamapori wakiwemo nyumbu na mamba katika hifadhi hiyo.

 

“Wanyama wanapenda kunywa maji ya mto Mara kwa sababu hayana magadi,” anasema Mhifadhi Utalii wa SENAPA, Geoffrey Kyando katika mahojiano maalumu na Mara Online News wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mara mwaka huu (2020) kwenye viwanja vya maonesho ya kilimo vya Mama Maria Nyerere, Butiama mkoani Mara.

 

Ikumbukwe pia kwamba wanyama kama vile iboko, mamba na viumbe hai wengine wanaochangia mvuto wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanaishi katika mto Mara.

 

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kushirikiana bega kwa bega na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani katika kudumisha utunzaji na uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti.

Mhifadhi Utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), Geoffrey Kyando akielezea umuhimu wa Mto Mara katika uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti wakati wa mahojiano na Mara Online News.

 

Mhifadhi Kyando anafarijika kuona kuwa SENAPA, FZS na wadau wengine wa uhifadhi wameendelea kushirikiana kwa hali na mali katika kuhakikisha ikolojia ya mto Mara na hifadhi hiyo inatunzwa kwa kiwango kinachostahili.

 

Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo, mto Mara umechangia kuiingiza Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwenye kumbukumbu ya maajabu saba ya urithi wa dunia kutokana tukio la uhamaji wa nyumbu ambao huvuka mto huo kila mwaka.

 

“Ifahamike pia kwamba mto Mara ni miongoni mwa vivutio vya kitalii vinavyoibeba hifadhi hii na umeibua fursa za uwekezaji katika sekta za utalii na uchumi,” anaongeza Mhifadhi Kyando.

 

Kyando anatumia nafasi ya mahojiano haya pia kualika watu kutoka ndani na nje ya Tanzania kutembelea SENAPA ili kuona mto Mara ulivyo kivutio na jinsi makundi ya wanyamapori aina ya nyumbu wanavyouvuka kwenda Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara nchini Kenya na kurudi Serengeti.

Sehemu nyingine ya nyumbu wakivuka Mto Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

Mto Mara unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui iliyo kwenye misitu ya Milima ya Mau ambapo maji ya mto huo hutiririka kupitia Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara, Kenya na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

 

Tanzania na Kenya imekuwa ikiadhimisha Siku ya Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara unaotiririsha maji Ziwa Victoria.

 

Mara Day ni zao la kikao cha 10 cha Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria kilichofanyika Kigali nchini Rwanda Mei 4, 2012 ambacho kiliazimia Siku hiyo iwe inaadhimishwa Septemba 15 kila mwaka.

 

Maadhimisho ya kwanza ya Mara Day yalifanyika 2012 nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo yalifanyika 2013.

 

Mbali na umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori, inakadiriwa kuwa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hutegemea uwepo wa Bonde la Mto Mara upande wa Tanzania na Kenya.

 

(Imeandikwa na Mara Online News, Butiama)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages