NEWS

Thursday 17 December 2020

Kiberenge alivyowabana watuhumiwa wa ujangili Serengeti

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamakendo, Joel Kiberenge akizungumza kikaoni. Aliyekaa ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Sereri mturi.


MWENYEKITI wa Kijiji cha Nyamakendo kilichopo Kata ya Machochwe, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Joel Kiberenge, ameeleza alivyopitia magumu ikiwemo kuhatarisha maisha yake katika kupambana na wakazi 120 wa kijiji hicho wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili, hasa uwindaji haramu kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

Wanakijiji hao wanatuhumiwa kujihusisha na uwindaji haramu wa wanyamapori wakiwemo nyumbu, nyati, viboko, kondoni na swala ndani ya hifadhi hiyo.

Nyati katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Nyumbu nadani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

“Serikali yangu ya kijiji imekuwa ya kwanza kutaja na kukamata wawindaji haramu. Kupitia mikutano ya hadhara ya wananchi nilichukua orodha ya watu wanaotajwa kujihusisha na uwindaji haramu katika hifadhini.

 

“Hatua hizo zilihatarisha maisha yangu hadi nikaomba msaada wa ulinzi wa usalama wangu kutoka wilayani, nililazimika kuhakikisha kuwa saa 12 jioni hainikuti nje ya nyumbani kwangu,” amesema Kiberenge katika kikao maalumu na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, viongozi wa kata na waandishi wa Mara Online News ofisini kwake, hivi karibuni.

 

Kiberenge amefafanua kuwa baadhi ya watuhumiwa hao wa uwindaji haramu wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria [polisi na mahakama] na wengine wamekimbia kijijini, miongoni mwao wamekwenda kujishughulisha na biashara ndogondogo (umachinga) katika miji mbalimbali nchini.

 

Alisema hatua hiyo imesaidia kupunguza uwindaji haramu na vitendo vingine vya ujangili katika hifadhi hiyo.

 

Mwenyekiti huyo amesema ameamua kuelekeza nguvu kubwa katika kukabiliana na majangili, hasa wawindaji haramu kwa kuwa uhifadhi wa wanyamapori ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

 

“Nilianza na vikao vya kueleza wanakijiji umuhimu wa uhifadhi maana walikuwa wamejenga dhana potofu juu ya uhifadhi kutokana na kauli za kichochezi kutoka kwa viongozi waliopita. Wananchi walichochewa kwamba wanyamapori ni mali yao iliyoshushwa na Mungu, hivyo ni haki yao kuwawinda.

 

“Lakini nimewataka wananchi kuondokana na dhaha hiyo potofu, nimewahamasisha kulinda hifadhi nikiamini kwamba ni jukumu la kiongozi kusimamia ulinzi wa rasilimali za nchi hii, tunashirikiana na diwani kuomba ushirikiano, nitataka tufanye kazi kama timu moja ili kuwezesha uhifadhi endelevu,” amesema Kiberenge.

 

Nao wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyamakendo, Maria Joseph na Daniel Marwa wamesema uwindaji haramu hauna faida yoyote zaidi ya kuwawaweka wahusika katika hatari ya kufungwa jela na hata kuuawa na wanyamapori wakali hifadhini.

 

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Serikali ya Kijiji cha Nyamakendo, Diwani wa Kata ya Machochwe, Joseph Mwegete, Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Victoria Makuru na Ofisa Ntendaji wa Kijiji hicho, Sereri Mturi, wameomba Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupitia idara yake ya Ujirani Mwema kuimarisha uhusiano wa hali na mali na wakazi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo ili kuwafanya wathamini uhifadhi.

 

Wamefafanua kwamba ujirani mwema uhusishe kuelimisha wanavijiji umuhimu wa uhifadhi na faida zake, lakini pia Hifadhi iongeze uwezeshaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi vijijini na ajira zinazowezekana kwa vijana kutoka maeneo hayo.

 

Wametaji miradi ya kijamii inayohitaji uwezeshaji kuwa ni pamoja na afya, elimu, barabara na maji kwa ajili ya malisho ya mifugo ya wanavijiji.

 

Kwa upande wa kijiji cha Nyamakendo, Mwenyekiti Kiberenge amesema kipaumbele chake cha kwanza ni ukamilishaji wa jengo la zahanati ya kijiji hicho lililojengwa kwa nguvu ya wananchi.

 

Akijibu hoja hizo, Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard, amesema idara yake hiyo na Hifadhi kwa ujumla haijasita kuendeleza ushirikiano na wanavijiji ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa uhifadhi kupitia mikutano ya hadhara.

 

Kuhusu uwezeshaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi, Hobokela amesema Hifadhi itaendelea kuwatengenezea fursa za ajira kwa kadri itakavyoweza ili wakazi wa vijiji jirani wanufaike zaidi na uhifadhi wa wanyamapori.

Kutoka kushoto waliosimama ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamakendo, Joel Kiberenge, Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji hicho, Maria Joseph na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Machochwe, Victoria Makuru.

 

“Tunapenda tutekeleza miradi mingi ili wananchi waone umuhimu wa uhifadhi, na ifahamike kwamba tunatekeleza miradi iliyoanzishwa na wananchi wenyewe kupitia SCIP (Support Community Initiated Projects). Mahitaji ni makubwa lakini azma yetu kubwa ni kuona wananchi wananufaika zaidi na uhifadhi,” amesema Mhifadhi huyo.

 

Akizungumzia ajira kwa vijana kutoka vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo, Hobokela amesema Hifadhi inaendelea na mikakati ya kutengeneza fursa hizo, lakini akataka wafahamu kwamba sio rahisi kila mtu kupata ajira hifadhini.

 

Hivyo, ameshauri vijana kubuni miradi ya kujiajiri wenyewe kama vile ufugaji (kuku na mbuzi) na kilimo (mfano cha mboga na matunda) itakayowawezesha kunufaika na fursa za masoko zinazopatikana hifadhini, kwenye hoteli na kambi za kitalii.

 

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni kivutio bora cha utalii na ilishaingizwa kwenye orodha ya maajabu saba ya urithi wa dunia. Lakini pia imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Zaidi Barani Afrika kwa miaka miwili mfululini (2019 na 2020).

 

(Imeandikwa na Mara Online News, Serengeti)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages