NEWS

Thursday 23 May 2024

RC Mtambi atatua mgogoro wa mpaka wa ardhi kijijini Rigicha- Serengeti



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake wilayani Serengeti jana.
----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
----------------------------------------


Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi jana alianza ziara yake katika wilaya ya Serengeti, ambapo alitatua mgogoro wa mpaka kijijini Rigicha.

Kanali Mtambi aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kufuata seheria, taratibu na maridhiano ya kifamilia na kijamii katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

“Ninaomba niwapongeze sana wananchi wa kijiji cha Rigicha, kwa busara na ustahimilivu wenu wa kusubiri kuutatua mgogoro huu kwa kufuata misingi ya haki na sheria, hongereni sana,” alisema Kanali Mtambi.

Kanali Mtambi aliwasikiliza wananchi kutoka familia moja waliokuwa wanagombea mpaka wa eneo pamoja na maombi ya kuhamisha njia ya muda mrefu ili kuruhusu shamba la familia kuwekewa mpaka.


Mwananchi akiwasilisha kero yake kwa RC Kanali Mtambi.
--------------------------------------------

Mgogoro huo ulitokana na Magdalena Francis kuomba kuhamisha barabara ya eneo hilo ipite pembezoni mwa shamba la familia yake, na baadaye kuanzisha mgogoro na Mgosi Magesa anayepakana naye wakigombea sehemu ya shamba hilo.

Hata hivyo, Kanali Mtambi alisuluhisha mgogoro huo na kusimamia uwekaji wa mpaka mpya wa barabara katika eneo hilo na kuwataka wanafamilia waliokuwa na mgogoro kushikana mikono kuashiria kuhitimishwa rasmi kwa mgogoro huo.

Baadaye alizungumza na wanakijiji na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Serengeti kuongeza watumishi katika zahanati ya Rigicha.

Aliitaka pia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (RUWASA) kukamilisha mradi wa maji katika eneo hilo.


Kanali Mtambi (kushoto) akimpa 
ofisa wa RUWASA maelekezo.
-------------------------------------------------

Kwa upande wake kiongozi wa familia iliyokuwa na mgogoro wa ardhi, John Francis Kisongo alisema eneo hilo ni la familia yao na babu zao walikuwa wanalima mashamba hayo na kwamba wanaogombania sasa ni warithi baada ya wamiliki wa awali kufariki dunia.

Kisongo aliwataka wanafamilia hao kuheshimu mpaka uliowekwa jana katika eneo hilo na kuwaomba kuendelea kuishi kwa amani kama ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kwa mgogoro huo.

Baada ya hapo, Mkuu wa Mkoa alikagua mradi wa maji wa Nyiberekela na kufanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya ya Serengeti, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Isenyi, kupokea na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa eneo hilo.

Katika ziara hiyo, Kanali Mtambi alifuatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati za Usalama Mkoa wa Mara na Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya hiyo, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wakuu wa taasisi za umma zilizopo wilayani Serengeti.

Mkuu wa Mkoa Kanali Mtambi anaendelea na ziara hiyo wilayani Serengeti leo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages