![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa shule za sekondari mjini Musoma jana. ------------------------------------------- |
Na Mwandishi Wetu
--------------------------
Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA), Mkoa wa Mara, kimetakiwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana shuleni.
Wito huo ulitolewa jana na Mkuu Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, wakati akifunga kikao cha TAHOSSA mjini Musoma.
Alikitaka chama hicho kuwahimiza wazazi na walezi waelewe wajibu wao katika kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa chakula wawapo shuleni na iwapo kuna changamoto, ni jukumu la wakuu wa shule kuziwasilisha kwa viongozi ili zipatiwe ufumbuzi.
“Mkoa wa Mara hakuna mwanafunzi atakayeshinda na njaa kwa kuwa mzazi au mlezi wake hataki kutimiza wajibu wa kumpatia chakula akiwa shuleni. Tutawachukulia hatua kwa wazazi watakaokataa kuchangia chakula kwa wanafunzi,” alisema.
Kiongozi huyo alipiga marufuku kwa shule kutoa chakula kwa njia ya ubaguzi kwa baadhi ya wanafunzi kuwaacha wengine wakihangaika eti kwa sababu tu wazazi ama walezi wao hawajachangia chakula hicho.
”Toeni taarifa kwa viongozi katika maeneo yenu ili wazazi jeuri wasiochangia chakula wachukulie hatua,” aliwaambia wakuu wa shule.
Kanali Mtambi aliwataka Wakuu wa Shule za Sekondari kutumia vizuri fursa iliyotolewa na Taasisi ya Pamoja Tuwalishe kwa kujenga majiko na stoo kwa mujibu wa maelekezo ya taasisi hiyo ili shule zote za mkoa wa Mara ziweze kupatiwa majiko banifu na sufuria zake ili kuleta uhakika wa wanafunzi wengi kupata chakula cha mchana shuleni.
Naye Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Makwasa Bulenga, aliwataka Wakuu wa Shule kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.
Akitoa neno la shukrani, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kirumi wilayani Butiama, Anna African Sarita, alisema walimu wanajitahidi kufuatilia wazazi na walezi wa wanafunzi kuchangia chakula mashuleni lakini wazazi wengi hawataki kuchangia kwa visingizio mbalimbali.
Aliahidi kwamba kwa kutumia kamati za shule, Wakuu wa Shule watawahamasisha wazazi kuweza kutumia nishati safi na majiko banifu ili wanafunzi waweze kupikiwa chakula katika mazingira salama na bila kuharibu mazingira.
Kikao hicho cha siku mbili kimefanyika kuanzia juzi na jana katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songe iliyopo Manispaa ya Musoma na kuwakutanisha Wakuu wa Shule za Sekondari 301 za mkoa wa Mara.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa aliwapongeza walimu waliofanikisha ufaulu wa wanafunzi wa Kidato cha Sita mwaka 2023 katika matokeo ya Mtihani wa Taifa.
Aliwataka Wakuu wa Shule kuongeza jitihada na kuwawezesha wanafunzi kufaulu mitihani yao, hususan kwa Kidato cha Pili na cha Nne ambapo amesema Mkoa wa Mara haufanyi vizuri sana katika mitihani ya Taifa kutokana na sababu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment