
Na Mwandishi Wetu, Tanga


Vijana katika Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Tanga wamefanya mazoezi (jogging) ya pamoja, ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kujenga na kuimarisha afya kwa Watanzania, hasa vijana.
Mazoezi hayo yalifanyika chuoni hapo jana Desemba 21, 2024, yakishirikisha vijana kutoka Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (COHAS) kilichopo jijini Tanga.
“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa, jogging hii pia ni harakati za kupambana na maradhi yasiyo ya kuambukiza na kujenga afya kwa wanachuo, maana mazoezi ni afya na afya ni mazoezi,” alisema Dkt Mwita Sospeter Mkami, Kaimu Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Tanga.

Dkt Mkami alisema mazoezi hayo pia ni maandalizi ya kuelekea TIA Tanga Festival itakayofanyika Januari 18, pamoja na TIA Marathon 2025.
Aliushukuru uongozi wa CCM Mkoa na Wilaya ya Tanga Mjini kwa kuwaunga mkono katika kufanikisha mazoezi hayo ya kihistoria kuelekea Bonanza la TIA Kampasi ya Tanga.
“Pia, ninamshukuru Mwenyekiti wa Mtaa wa Kange na Afisa Mtendaji wa Kata ya Maweni kwa ushiriki wenu katika jogging hii,” alisema Dkt Mkami.
Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhamasisha vijana kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kusoma kwa bidii na kuwa wabunifu.

“Jogging hii isiwe mwanzo wala mwisho. Pia, jitumeni, zingatieni masomo na kuwa wabunifu maana dunia ya sasa imejaa ushindani. Bila ubunifu elimu yako haitakuwa na maana katika soko la sasa, hasa kwenye zama hizi za sayansi na teknolojia na matumizi ya artificial intelligence (akili mnemba).
“Vijana mnapaswa kwenda na wakati ili msiachwe na wakati, bila kufanya hivyo utaishia kulaumu serikali kwamba ajira hakuna. Ubunifu wako ndiyo ajira yako,” Dkt Mkami alisisitiza.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Mara Press haitafanya kazi na online TV, blogs ambazo hazijasajiliwa TCRA – Mugini
>>Nyambari, Maswi wabeba harambee ya Kurya Social Group, zaidi ya milioni 20/- zapatikana Namba Tatu akimwakilisha mgeni rasmi
>>Basi la Kisire lapata ajali Magu, baadhi ya abiria wahofiwa kufa
>>TAMISEMI yatangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2025
No comments:
Post a Comment