NEWS

Sunday, 13 July 2025

Matokeo Kidato cha Sita 2025: Manga Sekondari wafanya ibada ya shukrani, DC Tarime, MNEC Gachuma washiriki



DC Tarime, Meja Edward Gowele (kulia), akikabidhi zawadi kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Editha Lazaro Nakei, wakati wa ibada ya shukrani kwa matokeo mazuri ya Mtihani wa Kidato cha Sita 2025, Ijumaa iliyopita. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, MNEC Christopher Gachuma.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Meja Edward Gowele na MNEC Christoper Gachuma wameshiriki ibada ya shukrani iliyoandaliwa na Shule ya Sekondari Manga kufuatia matokeo mazuri ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka huu wa 2025.

Ibada hiyo ambayo ilifanyika shuleni hapo Ijumaa iliyopita, ilihudhuriwa pia na viongozi wengine mbalimbali wa serikali, dini, bodi ya shule, walimu, wanafunzi na wazazi.

Meja Gowele ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu maendeleo ya sekta ya elimu katika wilaya hiyo, alitumia nafasi hiyo kuwapa walimu motisha na kuwatia moyo wanafunzi kuendeleza juhudi za kusoma za bidii.

Mbali na Shule ya Sekondari Manga, kiongozi huyo wa wilaya alizipongeza shule zote za kidato cha sita wilayani Tarime kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani huo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Manga, Mwalimu Editha Lazaro Nakei, alisema lengo kuu la ibada hiyo ni kumshukuru Mungu kwa matokeo mazuri ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita waliyopata mwaka huu, ambapo wanafunzi 235 walipata ufaulu wa daraja la kwanza, 164 daraja la pili na 11 daraja la tatu.

“Kwa miaka mitatu mfululizo shule yetu imepandisha ufaulu, hivyo hatuna budi kumshukuru Mungu, maana moyo usiona shukrani hukausha mema yote,” alisema Mwalimu Nakei.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Christopher Gachuma, alisema ni desturi yao kuwapongeza walimu kila wanapofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya taifa ya vidato vyote shuleni hapo.

Gachuma ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), alisema Bodi ya Shule inajivunia walimu wenye moyo wa kujituma kwa ajili ya taaluma ya shule hiyo.

Aliwahamasisha wanafunzi kukazania masomo akisema serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iko nao bega kwa bega kuhakikisha ustawi wa walimu na wanafunzi unaboreshwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, MNEC Christopher Gachuma akizungumza katika hafla hiyo.
----------------------------------------

Naye Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Tarime, Mwalimu Venance Chola Babukege, aliwapongeza walimu kwa kuwa mfano katika kusimamia nidhamu ya wanafunzi shuleni hapo, akisema nidhamu yao ndiyo imechangia kupata matokeo mazuri.

Afisa Elimu huyo aliahidi kuimarisha ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri katika mitihani ya taifa.
Afisa Elimu, Mwalimu Vence Chola Babukege akizungumza katika hafla hiyo.
-------------------------------------

Viongozi wa dini walioshiriki ibada hiyo ya shukrani ni pamoja na wachungaji kutoka Kanisa la EAGT Komaswa, FPCT Komaswa na Surubu, Katekista wa Kigango cha Surubu, Ustadhi wa Msikiti wa Komaswa, Mchungaji SDA Bukenye na Mlezi wa UKWATA Mkoa wa Mara, miongoni mwa wengine.

Viongozi hao wa kiroho waliwakumbusha wanafunzi umuhimu wa kuwa na hofu ya Mungu, maadili mema na bidii katika elimu.

Wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Manga ni mchanganyiko (wavulana na wasichana), na kidato cha tano na sita ni wasichana pekee.
Read Also Section Example

Unaweza pia kusoma:

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages