
Afisa Mendeleo ya Jamii kutoka Global Communities, Hillary Dashina, akiwasilisha mada ya mafunzo kwa wakulima wawezeshaji kwenye ukumbi wa Kituo cha Kilimo Mogabiri wilayani Tarime, wiki iliyopita. (Picha na Mara Online News)
------------------------------------------
Huenda uzalishaji wa mazao ukapaa na kuinua uchumi wa wakulima katika wilaya za Serengeti na Tarime mkoani Mara, baada ya wakulima wawezeshaji wa kujitolea katika wilaya hizo kujengewa uwezo na Shirika la Global Communities kupitia Mradi wa Pamoja Tuwalishe.
Lengo la mafunzo hayo ya siku nne, ni kuwapa wakulima maarifa ya mbinu bora za uzalishaji wa mazao, hata bila kutegemea maafisa kilimo, ambao wanakuwa na maeneo makubwa ya kuhudumia kwa wakati mmoja.
Kwa upande mwingine, wawezeshaji wengine wa jamii katika masuala ya vikundi vya kuweka na kukopa kutoka wilaya hizo, wamepewa mafunzo ya wiki moja - yanayolenga kuwasaidia wazazi kujipatia kipato ili kuweza kuwahudumia watoto wao wanapokuwa shuleni na nyumbani.
Mafunzo yote hayo yalitolewa wiki iliyopita katika kumbi mbili tofauti wilayani Tarime, wawezeshaji wakuu wakiwa Afisa Maendeleo ya Jamii, Hillary Dashina, Mtaalamu wa Kilimo, Dkt. Amithay Kuhanda, Afisa Mwezeshaji wa Jamii, Emmanuel Shukia na Sospeter Mgunda kutoka Global Communities, pamoja na Mwezeshaji wa Mafunzo ya Kidijitali, Salah Mwaitende kutoka Kampuni ya Jumsa Clubs.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha pia maafisa kilimo, wakiwemo Cosmas Karumuna kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Fulment Laurent kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ambao walipongeza Mradi wa Pamoja Tuwalishe, wakisema umekuwa mdau mkubwa katika halmashauri hizo katika kusaidia juhudi za serikali za kuhamasisha kilimo chenye tija.
“Mafunzo haya yatawasaidia wakulima wetu kuwa mabalozi kwa wale ambao wamewaacha vijijini, kuendeleza teknolojia ya kilimo ili kuzalisha kwa tija, kujitosheleza kwa chakula na kuongeza kipato kwa mkulima,” alisema Laurent.
Wakulima wawezeshaji takriban 40 - wanaume kwa wanawake waliopata mafunzo hayo wanatarajiwa kwenda kueneza mbinu bora za kilimo cha kisasa chenye tija na vikundi vya kuweka na kukopa fedha katika maeneo wanakotoka.
Aidha, uanzishaji wa mashamba darasa ya mazao aina ya mahindi, maharage na alizeti yanayohamasishwa na mradi mdogo wa Rick Steves II ndani ya Pamoja Tuwalishe, ni sehemu ya majukumu ya wakulima wawezeshaji waliopata fursa hiyo.
“Kupitia mafunzo hayo, wakulima wawezeshaji wamepata maarifa juu ya mbinu bora za kilimo zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi,” Dkt. Kuhanda aliiambia Mara Online News nje ya ukumbi wa mafunzo.
Kuhusu vikundi vya kuweka na kukopa fedha, wawezeshaji wa jamii wamejengewa mbinu bora za kuendesha vikundi hivyo, sambamba na utunzaji wa kumbukumbu kwa njia za kidijitali.
“Tumewafundisha wawezeshaji wa jamii namna ya kutunza taarifa kidijitali katika vikundi vya kuweka na kukopa, ikiwa ni pamoja na namna ya kuweka hisa zao na kutunza taarifa za mikopo,” alisema Salah.
Kupitia vikundi hivyo, wakulima wanaweza kuweka akiba na kukopa mtaji wa kuendeleza shughuli zao. Mfumo huo unawasaidia pia kujiandaa kwa dharura na kutotegemea mikopo ya riba kubwa kutoka kwa madalali, au taasisi zisizo rafiki.
Wakulima wawezeshaji wakiwa kwenye majadiliano wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoendeshwa na Shirika la Global Communities kupotia Mradi wa Pamoja Tuwalishe, kwenye ukumbi wa Kituo cha Kilimo Mogabiri wilayani Tarime, wiki iliyopita. (Picha na Mara Online News)
------------------------------------------
Wakulima wawezeshaji, Damali Nyahiri kutoka kata ya Mbogi wilayani Tarime na Paulina Mwita Chacha kutoka kata ya Machochwe wilayani Serengeti, wanasema mafunzo waliyopata yatasaidia kuwabadilisha wananchi wa wilaya hizo kuondokana na kilimo holela kisicho na tija.
‘Kutokana na mafunzo haya sasa tunaenda kuanza kilimo bora, na tayari nimeshawasiliana na wanajamii wenzangu - nimewambia nilikuwa kwenye mafunzo - wamefurahi na wanatamani sana niende kuwafundisha,” alisema Paulina.
“Kama kila familia itavuna vizuri na kuhifadhi vizuri, watoto wetu hawatakwenda shuleni wakiwa na njaa,” alisema Damali na kuongeza “Kwa mafunzo tuliyopata, sasa tuna uhakika wa kutafikia lengo la kuwa na jamii inayojitosheleza kwa chakula.”
Naye mkulima mwezeshaji kutoka kata ya Kisaka wilayani Serengeti, Edward Shitunguru, alisema “Haya mafunzo yatakuwa msaada mkubwa kwa wakulima kwa sababu kuna upungufu wa wataalamu wa kilimo kwenye vijiji na kata. Hivyo sisi tutakuwa msaada, tutasaidiana na maafisa kilimo wachache waliopo kuwapa wakulima mbinu za kilimo cha kisasa.”
Lengo kuu la Shirika la Global Communities kupitia Pamoja Tuwalishe na mradi mdogo wa Rick Steves II, ni kuhakikisha kuwa uzalishaji wa chakula na lishe vinaimarishwa katika jamii - kuanzia nyumbani hadi shuleni.
Wakati wazazi wakihamasishwa kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni ili kuwawezesha kusoma kwa amani, shule nazo zinahamasishwa kuwa na mashamba darasa kwa ajili ya kufundisha wanafunzi kilimo cha kisasa chenye tija.
No comments:
Post a Comment