
Jenista Joakim Mhagama enzi za uhai
Waziri wa zamani wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Jenista Joakim Mhagama, amefariki dunia Alhamisi, Desemba 11, 2025.
Taarifa iliyotolewa leo na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, haikueleza chanzo cha kifo cha mbunge huyo wa muda mrefu wa Peramiho.
Mwanamana huyo aliitumikia serikali katika nyadhifa mbalimbali akianzia kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia shughuli za Bunge katika Serikali ya Rais John Magufuli.
Pia, alikuwa Waziri wa Afya katika Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan hadi alipoachwa kwenye Baraža la sasa la Mawaziri, baada ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.
Mbunge huyo, ambaye alikuwa mhamasishaji maarufu wa nafasi ya mwanamke katika uongozi, alizaliwa Juni 23, 1967 na alisoma taaluma ya ualimu.
Taarifa ya Bunge imeeleza kuwa uongozi wa mhimili huo wa dola unashirikiana na familia ya marehemu huyo katika maandalizi ya mazishi.
Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge huyo wa Peramiho.
Katika salamu zake za rambirambi alizomtumia Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Rais Samia amesema Mhagama kwa miaka 38 alikuwa mwanachama mahiri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mnasihi wa watu wengi katika siasa na maisha.
No comments:
Post a Comment