
Nyati
Mara Online News
Mkulima na mkazi wa kijiji cha Manuna, Marungu Chacha Ruhuro, ameripotiwa kufariki dunia baada ya kushambuliwa na nyati katika kijiji jirani cha Wagete, wilayani Serengeti, mkoani Mara.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Wagete, Juma Samwel Sabuda, amethibitisha tukio hilo akisema lilitokea Jumanne, Desemba 9, 2025 saa tano asubuhi, wakati Ruhuro na wenzake kadhaa wakijaribu kumfukuza mnyama huyo kijijini.
“Alipoteza maisha akiwa anapatiwa matibabu katika zahanati ya kijiji, baada ya kushambuliwa kwa kuchotwa na kukanyagwa na nyati,” Sabuda ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu, Jumatano, Desemba 10, 2025.
Pia, mapema saa mbili asubuhi ya siku hiyo, mnyamapori huyo ambaye anasadikiwa kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti, anadaiwa kumshambulia na kumjeruhi mwanakijiji mwingine ambaye kwa sasa anaendelea kupata matibabu.
Hata hivyo, Sabuda ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa, maofisa wa Idara ya Wanyamapori kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti walifika kijijini hapo na kufanikiwa kumuua kwa risasi nyati huyo.
“Baada ya kumuua kwa kumpiga risasi, walimchinja na kugawa baadhi ya nyama zake kwa wananchi, na nyingine kikiwemo kichwa waliondoka nazo kama ushahidi,” amesema.
Aidha, maofisa hao waliahidi kugharimia mazishi ya mwananchi aliyepoteza maisha, pamoja na kuwapa ndugu husika kifuta machozi, kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kijiji.
No comments:
Post a Comment