
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika kilele cha Maonesho ya Nane Nane Kitaifa na Kimataifa jijini Dodoma jana.
Dodoma
-------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo (NAESA) unatekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi, huku ukizingatia dhana ya ugatuaji wa madaraka, maarufu kama D by D.
Rais Samia alitoa agizo hilo Agosti 08, 2026 wakati wa kufunga rasmi Maonesho ya Nane Nane Kitaifa na Kimataifa ya mwaka huu yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma.

Rais Samia akisililiza maelezo kutoka kwa mmoja wa waoneshaji kutoka nje ya Tanzania walioshiriki katika maonesho hayo
Aidha, Rais Samia aliielekeza OWM-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kushughulikia na kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Alisisitiza kuwa makundi hayo yote yana umuhimu mkubwa katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo ni muhimu kuweka mazingira yatakayoyawezesha kufanya shughuli zao kwa amani na tija.

Rais Samia akiwa kwenye usukani wa trekta la kilimo wakati wa kilele cha maonesho hayo
Kwa upande wake Naibu Katibu OWM-TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya, Prof. Tumaini Nagu, alisema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao, hususan kupitia fursa zinazotolewa na Serikali za Mitaa.
“Tumefanya vizuri kupitia mikopo ya halmashauri kuwafikia wananchi wengi na kuongeza uzalishaji, lakini bado kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi kwa kuwafikia vijana wengi, kina mama wengi na watu wenye ulemavu ili waingie katika mnyororo mzima wa uzalishaji,” alisema Prof. Nagu.
Alisema kuongeza tija katika kilimo hakupaswi kuishia katika uzalishaji wa mazao pekee, bali pia kuhusisha hatua zote za mnyororo wa thamani, ikiwemo uzalishaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji na upatikanaji wa masoko.
Prof. Nagu alisema Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, kutoa elimu, kuonesha teknolojia na ubunifu katika uzalishaji pamoja na kujadili fursa zinazoweza kuongeza tija na thamani katika sekta ya kilimo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, Maonesho ya Nane Nane ya mwaka huu yamewashirikisha waoneshaji 1,168, wakiwemo 25 kutoka nje ya Tanzania, huku wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi 282,206 wakishiriki katika maonyesho hayo.
Kaulimbiu ya Maoneshoy a Nanenane 2026 inasema: “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050.”
No comments:
Post a Comment