NEWS

Saturday, 29 August 2026

Shule ya Odikwa yasherehekea Mahafali ya Darasa la Saba na Awali 2026, yaahidi matokeo bora



Viongozi na walimu wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa darasa la saba wakati wa mahafali ya Shule ya Odikwa yaliyofanyika jana Ijumaa, Agosti 28, 2026. Aliyevaa suti nyeusi waliokaa ni Padre Cleophace Samwel Sabure ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.

Na Godfrey Marwa
Rorya
------------

Shule ya Awali na Msingi Odikwa iliyopo katika wilaya Rorya mkoani Mara, imesherehekea Mahafali ya Nne ya Darasa la Saba na Mahafali ya Nane ya Darasa la Awali.

Mahafali hayo yalifanyika shuleni hapo jana Ijumaa, Agosti 28, 2026 sambamba na harambee ndogo iliyoongozwa na Padre Cleophace Samwel Sabure ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Sehemu ya matukio ya wahitimu wa darasa la saba na walimu wao wakati wa mahafali hayo
Wahitimu wa darasa la awali wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mahafali hayo

Padre Sabure aliipongeza shule hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma, na kuiahidi ushirikiano na wadau mbalimbali wa elimu ili kuboresha zaidi mazingira kujifunzia na kufundishia.

"Naupongeza uongozi wa shule hii kwa matokeo bora kama nilivyosikia kwenye taarifa, faida mojawapo ya elimu ni connection (kiunganishi) cha watu mbalimbali, wazazi tuwekeze huko.

"Tutaendelea kushirikiana... katika maisha changamoto haziepukiki, tutazifanyia kazi kwa ushirikiano wa wadau na jamii ili kuhakikisha tunawapa watoto elimu iliyo bora,” alisema Padre Sabure.

Katika harambee, Padre Sabure alichangia shilingi milioni 1.5 na kuungwa mkono na Bodi ya shule hiyo kwa shilingi milioni 2.9, huku wazazi na wadau wengine wakimsindikiza kwa michango ya fedha taslimu na saruji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Odikwa, Mwalimu Hagai (kulia), akimkabidhi cheti cha shukrani.

Awali, Mkurugenzi wa shule hiyo, Mwalimu Jacob Nguka Ogola, alimshukuru mgeni rasmi na wazazi kwa ushirikiano wa dhati unaoiwezesha kuendelea kufanya vizuri kitaaluma.

"Ninaamini mnachokitaka Odikwa sio madaraja B na C, ni A, hicho ndicho ninachowaahidi kwamba watoto tunawandaa, lakini sio hapa tu, na huko wanakoenda wanapata one ya 7 na 8, waliomaliza hapa ni mashahidi.

"Tunaendelea kuwashukuru wazazi mnaoendelea kutuamini na kutuona kama chaguo sahihi. Wito wangu, tuendelee kuwahudumia Watoto. Odikwa tunaamini mtoto akiandaliwa kiroho, kimwili na kiakili, 'future’ yake itakuwa nzuri,” alisema Mkurugenzi Ogola.

Mwakilishi wa Kanisa Katoliki (aliyeshika kipaza sauti), Mkurugenzi Ogola (kulia) na wengine wakifurahia jambo wakati wa mahafali hayo.

Kwa mujibu wa Mwalimu Ogola, Shule ya Awali na Msingi na Odikwa yenye mchepuo wa Kiingereza, imeendelea kupata matokeo bora kitaifa kwa darasa la saba na la nne.

Alisema shule hiyo ina miundombinu bora, ikiwemo vyumba vya madarasa, mabweni, bwalo, jiko na nyumba za watumishi.

Pia, alisema shule ina umeme, maji ya uhakika, walimu bora wenye sifa na magari ya kusafirisha wanafunzi kwa kipindi chote cha masomo.

Mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa darasa la saba


Mgeni rasmi akiendelea kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa darasa la saba


Mzazi akimlisha mhitimu wa darasa la saba keki


Mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mhitimu wa darasa la awali shuleni hapo

Mkurugenzi Ogola alitaja baadhi ya mafanikio makubwa kitaaluma ambayo shule hiyo imepata kuwa ni watahiniwa wa darasa la saba wote walipata ufaulu wa daraja A mwaka 2025.

Alisema matokeo bora yameiwezesha shule hiyo kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kwa miaka mitano mfululizo (2020-2025 katika mitihani ya taifa ya darasa la nne.

"Naipongeza Bodi ya Shule hii kwa usimamizi mzuri, matokeo yameendelea kuwa mazuri, tunataka shule ya Odikwa iwe ya kwanza kimkoa mwaka kesho,” alisema mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo.

Mgeni rasmi Padre Sabure (aliyevaa suti nyeusi), Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Odikwa, Mwalimu Hagai (aliyeshikilia mtoto, Mkurugenzi wa shule hiyo, Mwalimu Ogola na wengine wakifurahia picha ya pamoja wakati wa mahafali hayo. (Picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages