
Waziri wa Madini wa Tanzania, Anthony Mavunde (kulia) na Waziri wa Ardhi na Maliasili wa Ghana, Emmanuel Armah-Kofi Buah, wakisalimiana kwa furaha walipokutana jijini Accra, Oktoba 21, 2026.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Ghana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo waweze kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa madini na usimamizi wa rasilimali hiyo.
Amesema wakati umefika kwa Afrika kuacha kuwa chanzo cha malighafi kwa viwanda vya nje, badala yake kutumia utajiri wake wa madini kujenga viwanda ndani ya nchi, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi wake.
Waziri Mavunde aliyasema hayo Oktoba 21, 2026, katika kikao cha pande mbili (bilateral meeting) kati yake na Waziri wa Ardhi na Maliasili wa Jamhuri ya Ghana, Emmanuel Armah-Kofi Buah, kilichofanyika jijini Accra.
Mawaziri hao hao walijadili fursa za kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na maendeleo ya sekta ya madini kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Mavunde alisema ni wakati muafaka sasa serikali za nchi hizo kuwaangalia wachimbaji wadogo kwa jicho la uwezeshaji ili waendelee kushiriki na kuchangia kikamilifu maendeleo ya uchumi kupitia sekta ya madini.
Alisisitiza kwamba kwa muda mrefu nchi za Afrika zimekuwa zikifanya kazi kwa kujitenga katika sekta ya madini, huku rasilimali kama dhahabu, shaba, grafiti, lithiamu na madini mkakati zikisafirishwa nje ya bara hilo bila kunufaisha kikamilifu uchumi wa nchi zinazozalisha madini hayo.
“Enzi ambazo Afrika inafanya kazi kama ghala la malighafi kwa mataifa mengine lazima ziishe, na lazima ziishe sasa,” alisisitiza Waziri Mavunde.
Alieleza kuwa nguvu ya Tanzania na Ghana haipaswi kuishia katika uchimbaji wa madini, bali pia katika kuunganisha utaalamu, teknolojia utafiti na uwezo wa kujenga mifumo ya uzalishaji na uongezaji thamani ndani ya Afrika.
Alisema ushirikiano huo unapaswa kuelekezwa katika maeneo muhimu, ikiwemo uongezaji thamani wa madini kupitia kuyeyusha, kusafisha, kuchakata na kuzalisha bidhaa za viwandani, badala ya kutegemea mauzo ya madini ghafi.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, hatua hiyo itasaidia kubakiza mitaji ndani ya nchi, kukuza uwezo wa viwanda vya ndani na kutengeneza ajira zenye tija kwa vijana wa Afrika.
Kuhusu utafiti wa kijiolojia, alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Ghana kubadilishana utaalamu, teknolojia na taarifa za kijiolojia ili kuimarisha uwezo wa kutambua rasilimali zilizopo, kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kujadiliana mikataba ya uwekezaji kwa kujiamini zaidi.
Alisema nchi za Afrika zinapaswa pia kuimarisha ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini ili wananchi wasibaki kuwa wafanyakazi pekee migodini, bali pia waweze kuwa wamiliki wa biashara, wawekezaji, wasambazaji wa bidhaa, huduma na wazalishaji wa bidhaa zinazotokana na madini.
Waziri Mavunde aliipongeza Gahana kwa hatua ilizochukua katika kuwezesha wachimbaji wadogo, akieleza kuwa Tanzania inaendelea kujifunza kutokana na uzoefu huo, huku ikilenga kujifunza namna Sheria ya Madini na Tume ya Madini ya Ghana zinavyosimamia shughuli za sekta hiyo, ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa madini katika nchi hizo mbili.
Kwa upande wa uwekezaji, Mavunde alizitaka kampuni na washirika wa kimataifa kuelekeza uwekezaji wao katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini, miundombinu na shughuli za kuongeza thamani ndani ya Afrika, huku wakizingatia mikataba yenye manufaa ya haki kwa nchi mwenyeji na wananchi wake.
Aidha, alimwalika waziri mwenzake wa Ghana na ujumbe wake kutembelea Tanzania miezi ijayo, ili kuendeleza mazungumzo na kuweka mifumo rasmi ya ushirikiano, ikiwemo kuanzisha vikundi kazi vya kitaalamu vya pamoja kati ya wizara za madini za nchi hizo mbili.
Alisema Tanzania na Ghana zina nafasi ya kuwa mfano wa ushirikiano wa kikanda katika kubadilisha utajiri wa madini kuwa maendeleo ya viwanda na ustawi wa wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inaelekea kwenye matumizi ya teknolojia na nishati safi yanayohitaji madini mkakati.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi na Maliasili wa Jamhuri ya Ghana, Emmanuel Armah-Kofi Buah, alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano badala ya kutegemea juhudi za kila nchi pekee katika kuendeleza sekta ya madini.
Buah alisema uzoefu wa kihistoria unaonesha kuwa utajiri wa rasilimali za Afrika haujawanufaisha kikamilifu wananchi wake kutokana na kuendelea kuuza malighafi bila kuzichakata na kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa ndani ya bara hilo.
Alieleza kuwa uongezaji thamani wa rasilimali ni msingi wa kujenga viwanda, kutengeneza ajira na kuinua maisha ya wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa Tanzania na Ghana kubadilishana uzoefu na mikakati iliyofanikiwa katika usimamizi wa sekta ya madini na kubainisha umuhimu wa mikataba ya madini kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazozunguka migodi.
Waziri Buah alitolea mfano wa mikataba ya maendeleo ya jamii inayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki katika matokeo ya uwekezaji wa madini.
No comments:
Post a Comment