
Tumbaku kavu
Na Mwandishi Wetu
--------------------------
Bei ya tumbaku imeshuka baada ya uzalishaji wa zao hilo kuongezeka na kuzidi mahitaji duniani, Gazeti la Sauti la Mara linaripoti.
Taarifa zinasema uzalishaji wa tumbaku kwa mwaka jana ulifikia takribani tani bilioni 5.8 didhi ya tani bilioni 5.2 ambazo ni mahitaji ya zao hilo kwa dunia nzima.
Hali hiyo imesabisha bei ya zao hilo kuporokoma kutoka dola za Marekani mbili na senti kumi (USD 2.1) kwa kilo moja mwaka jana hadi dola moja na senti 95 (USD 1.95) kwa kilo moja mwaka huu.
Hata hivyo, Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) imesema inaendelea kuweka mikakati kukabiliana na changamoto hiyo ili kulinda maslahi ya wakulima wa tumbaku nchini.
“Ni kweli kuwa bei ya tumbaku imeshuka lakini si Tanzania tu, ni duniani kote,” Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Stanely Mnozya, alisema katika mahojiano na Gazeti la Sauti ya Mara Ijumaa iliyopita.
Aidha, kwa sasa TTB inafanya juhudu za kutafuta wateja kwa ajili ya kununu akiba (stock) ya tumbaku iliyopo - ambayo ni takribani tani 33,000.
Mkurugenzi huyo wa TTB alikuwa akizungumzia malalamiko kuhusu kushuka kwa bei ya tumbaku katika maeneo ya mkoa wa Mara yanayolima tumbaku, hususan wilaya ya Serengeti.
Alisema “Ni kweli mwaka jana bei ilikuwa juu lakini mwaka huu imeshuka baada ya uzalishaji wa tumbaku duniani kuwa mkubwa zaidi mahitaji.”

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Stanely Mnozya.
Mnozya alisema TTB inahakikisha kuwa bei ambayo wakulima wanauza tumbaku inakuwa juu ya gharama walizotumia kwenye uzalishaji. “Bei iliyopo kwa sasa ipo juu ya gharama za uzalishaji,” alisema.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Mnozya alisema majadiliano ya wadau wa zao hilo yanaendelea ili kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji kama vile pembejeo, miongoni mwa mambo mengine. “Tunataka bei ya uzalishaji ishuke, huwezi kupambana na bei,” alisisitiza.
Alisisitiza kuwa kwenye mikakati ya kupunguza gharama za pembecheo, hasa mbolea pamoja na ubora katika uzalishaji wa zao hilo kupewa kipaumbele.
Wilaya ya Serengeti inaongoza kwa uzalishaji wa zao la tumbaku katika mkoa wa Mara, ikifuatiwa na Tarime.
Taarifa zinaeleza kuwa tatizo limekuwa zaidi kwa wafanyabiashara wa tumbaku ambao walinunua kwa wakulima kwa bei kubwa wakitarajia kuwa bei yake itaendelea kuwa kubwa kwenye soko la dunia.
“Shida kubwa ni kwamba kuna wale gorogoro walikuwa wananunua kwa bei wakijua hali itakuwa kama mwaka jana. Sasa bei imeshuka na wao walinunua kwa gorogoro kwa bei kubwa,” kilieleza chanzo chetu kutoka wilayani Serengeti juzi.
Mmoja wa wakulima wa tumbuku ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema gharama za uzalishaji zikipungua bado wataendelea na kilimo hicho.
“Hali siyo mbaya lakini pembejeo kama mbolea zikipungua bei tutaendelea na kilimo cha tumbaku vizuri,” alisema.
No comments:
Post a Comment