NEWS

Wednesday, 25 November 2026

Nyumba mpya zilizojengwa kupitia CSR Barrick zachangia kuboresha huduma Kituo cha Afya Nyangoto



Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyangoto, Abduladhimu Sued Ally, akiwaonesha waandishi wa habari nyumba mpya za watumishi zilizojengwa kituoni hapo na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Na Mwandishi Wetu
Tarime
--------------

Uwezo wa daktari au muuguzi kufika haraka kumhudumia mgonjwa sasa umeongezeka baada ya watumishi watano kuhamia katika nyumba mpya zilizojengwa ndani ya eneo la Kituo cha Afya Nyangoto kinachofahamika pia kwa jina la Sungusungu.

Ujenzi wa nyumba hizo tatu, zikiwemo mbili pacha, unatajwa kuimarisha mazingira ya utoaji wa huduma, zikiwemo za dharura kwa wakati katika kituo hicho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Wadau wanataja ujenzi wa nyumba hizo za kisasa kuwa ni uwekezaji muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa kituo hicho, Abduladhimu Sued Ally, kuishi karibu na kituo cha kazi kunawezesha madaktari na wauguzi kutoa huduma kwa wakati hata kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura hata nyakati za usiku.

“Watumishi waliokuwa wanaishi mbali na kituo sasa wanaishi hapa na wanatoa huduma za matibabu kwa wakati na muda wowote,” Sued anawambia waandishi wa habari waliotembelea kituoni hapa hivi karibuni.

Anasisitiza kuwa ujenzi wa nyumba hizo umeleta mabadiliko chanya katika mazingira ya kazi na maisha ya watumishi waliohamia, kwani umewawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Anasema kwa sasa watumishi wanaoishi katika nyumba hizo wanafurahia mazingira rafiki, hali inayochochea uwajibikaji, ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kaimu Muuguzi Mfawidhi, Sued, akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo.

Ujenzi wa nyumba hizo umegharimu shilingi zaidi ya milioni 300 zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Wananchi wanaopata huduma katika Kituo cha Afya Nyangoto wanasema mgodi huo umekuwa na mchago mkubwa katika kuboresha huduma za matibabu kituoni hapo.

“Kampuni hii [Barrick North Mara] imetusaidia kwa kiwango ambacho hatukutegemea, sasa hivi mgojngwa akija hapa wakati wowote anapata huduma,” anasema Gabriel Nyankomo, mmoja wazee maarufu katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Catherene Enock, mmoja wa ndugu za wagonjwa waliozungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, anasema huduma za afya zinahitaji watumishi na mazingira rafiki ya kazi, hivyo kuwaweka karibu na kituo cha kutolea huduma kutachangia kuepusha vifo visivyo vya lazima.

Anasema ujenzi wa nyumba hizo una maana kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo kutokana na kuimarisha kwa huduma za afya, hasa pale wanapokabiliwa na changamoto zinazohitaji uangalizi wa haraka.

Catherene Enock akizungumza na waandishi wa habari

Naye Diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba, anasema miradi inayotekelezwa nchini ya mpango wa CSR wa Mgodi wa Barrick North Mara ina manufaa makubwa kwa jamii inayozunguka mgodi huo.

“Mfano, ujenzi wa nyumba hizi umesaidia watumishi kuwa jirani na kituo cha kazi kwa ajili ya kuhudumia wananchi,” Bogomba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ya Barrick North Mara, anawambia waandishi wa habari.

Diwani Rashid Bogomba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CDC

Hivyo, Kaimu Muuguzi Mfawidhi, Sued, na wananchi wa maeneo hayo wanaushukuru mgodi huo kwa kushirikiana na serikali kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

Wanakiri kuwa uwekezaji kwenye nyumba hizo za watumishi umekuwa na matokeo chanya katika utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho.

Hata hivyo, Sued anahitimisha mazungumzo hayo kwa kuomba Mgodi wa Barrick North Mara kuangalia uwezekano wa kusaidia ukarabati wa nyumba za zamani za watumishi zinazohitaji matengenezo kituoni hapo.

Sehemu ya mbele ya Kituo cha Afya Nyangoto. (Picha zote na Sauti ya Mara)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages