NEWS

Tuesday, 17 November 2026

Utendaji usioridhisha wawaponza watumishi wanne Rorya, DC Mabula aagiza wahamishwe vituo vya kazi



Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Stanslaus Mabula, akizungumza na wananchi kijijini Ruhu.

Na Mwandishi Wetu
Rorya
-------------

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Stanslaus Mabula, ameagiza kuhamishwa kwa watumishi wa umma wanne katika kijiji cha Ruhu na kata ya Kyang’ombe, kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za afya zisizoridhisha na kushuka kwa taaluma katika Shule ya Msingi Ruhu.

Maelekezo hayo yanahusisha kuhamishwa kwa Mganga Mfawidhi na muuguzi mmoja wa Zahanati ya Ruhu, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kyang’ombe na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ruhu.

Kuhusu Mwalimu Mkuu huyo, DC Mabula ameelekeza kufanyiwa tathmini ya kiutendaji ili kubaini hatua stahiki, ikiwemo uwezekano wa kushushwa cheo au kuhamishwa kituo cha kazi.

Akitoa maelekezo hayo Novemba 12, 2026, baada ya kutembelea kijiji hicho na kusikiliza kero za wananchi, Mabula alikemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea, akionya kuwa uzembe na kutowajibika kwa watumishi wa umma kunadhoofisha huduma na kupunguza imani ya wananchi kwa serikali yao.

Alisisitiza kuwa serikali inahitaji watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu, nidhamu, uwajibikaji na ufanisi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kujivunia maeneo wanayoishi.

Aidha, DC Mabula aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za kweli kuhusu uzembe na mapungufu katika utoaji wa huduma za umma, akisisitiza kuwa taarifa hizo zisiwe za kusingizia watumishi ili hatua zinazochukuliwa ziwe za haki bila kumuonea mtu yeyote.

Taarifa zaidi zinasema watumishi walioelekezwa kuhamishwa wamehudumu katika vituo hivyo kwa miaka zaidi ya 10. Hivyo, hatua iliyochukuliwa inalenga kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa DC Mabula, serikali inaendelea kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora, kwa wakati na kwa haki.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages