NEWS

Saturday, 21 November 2026

Wadau wa kilimo wataka mabaraza ya ardhi yawezeshwe kusimamia matumizi ya ardhi, utunzaji mazingira



Mratibu wa Programu ya ASILIB-CC 2026–2028 inayotekelezwa na MVIWANYA, Joel Nguvava, akizungumza katika kongamano la wadau wa kilimo na mazingira kutoka wilaya za Tarime na Serengeti lililofanyika mjini Tarime, Novemba 20, 2026.

Na Godfrey Marwa
Tarime
-----------

Halmashauri zimeshauriwa kutenga sehemu ya bajeti zake kwa ajili ya kuwezesha mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata na wilaya kusimamia matumizi bora ya ardhi na utunzaji wa mazingira badala ya kujikita katika kushughulikia migogoro pekee.

Ushauri huo ulitoletwa na wadau wa sekta za kilimo na mazingira kutoka halmashauri za wilaya za Tarime na Serengeti, mkoani Mara, Novemba 20, 2026, wakati wa kilele cha kongamano la siku tatu lililofanyika mjini Tarime.

Kongamano hilo liliandaliwa na kuendeshwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA) unaotekeleza Programu ya ASILIB-CC 2026–2028 katika wilaya hizo, ili matumizi endelevu ya rasilimali za umma, ikiwemo ardhi, vyanzo vya maji na misitu.

Washiriki wa kongamano hilo walikuwa madiwani, wakulima, maafisa kilimo, mazingira, maendeleo ya jamii na wadau wa sheria na haki za binadamu.

Mkulima akichangia mada katika kongamano hilo

"Tukishirikisha watunga sera na wataalamu wa mipango tukapendekeza kila halmashauri itenge asilimia mpaka mbili, angalau hata milioni 20 kuwezesha mabaraza ya ardhi na majukwa ya wakulima tutapata matokeo,” alisema Matoke Joseph ambaye ni diwani na mkulima kutoka wilayani Serengeti.

Diwani wa Kata ya Uwanja wa Ndege kutoka Serengeti, Mwita Matoke, aliunga mkono hoja hiyo akisema "Tukitaka haya mabaraza ya ardhi yaendelee lazima halmashauri tukubali kuyasapoti, hawa ni fursa kwa wakulima.”

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu Tarime la Tuwakomboe Paralegal (TPO), Bonny Matto, alishauri utengaji wa bajeti za mabaraza ya ardhi uende sambamba na mpango mkakati wa matumizi ya ardhi.

Mkurugenzi wa TPO, Bonny Matto, akizungumza katika kongamano hilo. (Picha zote na Mara Online News)

Kwa upande wake Joel Nguvava ambaye ni Mratibu wa Programu ya ASILIB-CC 2026–2028 inayotekelezwa na MVIWANYA chini ya ufadhili wa Shirika la Vi Agroforestry, aliiomba serikali kuendelea kuyajengea mabaraza ya ardhi uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

"Tunaomba serikali iendelee kutoa elimu na kuimarisha mabaraza ya ardhi ya wilaya, kata na vijiji ili kusimamia matumizi endelevu ya ardhi badala ya kushughulikia migogoro pekee,”

Aidha, Nguvava alisisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kusimamia sheria, taratibu na miongozo iliyopo katika kuhakikisha vyanzo vya maji na rasilimali zote za umma zinatumika kwa manufaa ya jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages