NEWS

Friday 20 March 2020

PARACHICHI ZILIVYOMPAISHA BINTI MHITIMU WA SHAHADA YA SHERIAWAKATI wahitimu wengi wa vyuo vikuu  wakiamini kuajiriwa ndio njia pekee inayoweza kuwatoa kimaisha, hali ni tofauti kwa Veronica Bilali maarufu kwa jina la VeeMoney.

Bilali ambaye ana shahada ya sheria ni mkazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara. Sasa hivi anachomoza kama mjasiriamali na mwanamitindo anayeng’ara siku hadi siku wilayani Tarime.

Mwanadada vee money alizaliwa mwaka 1991, alitumia fursa ya kuuza parachichi kuanza safari yake ya ujasiriamali.

“Baada ya kukaa nyumbani mwaka mzima bila kazi, ndipo nikaamua kuuza parachichi ambapo nilikuwa nikizisafirisha kutoka Tarime kwenda kuziuza jijini Mwanza,” anasema Bilali katika mahojiano maalumu na  Mara Onlne news ofisini kwake, wiki iliyopita.

Tarime ni miongoni mwa maeneo ya mkoa wa Mara yanayozalisha parachichi kwa wingi. Hivyo, Bilali alitumia fursa hiyo kupata mtaji na kuingia rasmi katika sekta ya mapambo.

Kutokana na ubora wa kazi zake, Bilalia ameanza kupata kazi za kupamba sherehe mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“Hivi sasa ninapata wateja wa kupambiwa sherehe mbalimbali katika maeneo tofauti ya Tarime na nchi jirani ya Kenya. Hata hivi karibuni sisi VeeMoney tulipata kazi ya kupamba jijini Nairobi, Kenya,” anaeleza.

Bilali anafafanua zaidi kwamba alilazimika kuanza kazi ya ujasiriamali akiwa mwanafunzi baada ya baba yake kupata ajali iliyomsababisha  kushindwa kugharimia mahitajii ya masomo yake.

“Nilianza kuuza nguo na cheni, nikafanikiwa kupata pesa ya kulipa karo ya mwaka mzima. Ninamshukuru Mungu kuwa hali hiyo ilinifanya kupenda kazi ya ujasiriamali badala ya kuajiriwa,“ anasema Bialali.

Kujiamini kwa Bilali kumemsukuma kujiita Malkia wa Nguvu baada ya kuamini kuwa anaweza kukabiliana na changamoto za maisha na kusonga mbele kama mwanamke.

Mbali ya shughuli za mapambo, Bilali anafanya biashara ya kuuza nguo za kisasa na vinywaji mbalimbali.

Ndoto yake kubwa

Bilali anasema ndoto yake kubwa ni kuwa mwanamitindo bora ndani na nje ya Tanzania siku za usoni.


“Ukiangalia mavazi yangu ni ya kimitindo, lakini moja ya ndoto yangu ni kuwa designer (mwanamitindo) maarufu na kutoa pia fursa nyingi za ajira kwa vijana wa kike,“ anasema Bilali.

Ujumbe wa Bilali kwa wanawake wa wilayani Tarime ni kuthubutu kuwa wajasiriamali kwa kutumia fursa zilizopo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Lakini pia sisi kama wanawake tunapaswa kupendana na kufanya kazi kwa ushirikiano na kuondokana na dhana ya utegemezi,” anasema Bilali kuhitimisha mahojiano haya.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages