WAKATI
wahitimu wengi wa vyuo vikuu wakiamini
kuajiriwa ndio njia pekee inayoweza kuwatoa kimaisha, hali ni tofauti kwa
Veronica Bilali maarufu kwa jina la VeeMoney.
Bilali
ambaye ana shahada ya sheria ni mkazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara. Sasa
hivi anachomoza kama mjasiriamali na mwanamitindo anayeng’ara siku hadi siku
wilayani Tarime.
Mwanadada
vee money alizaliwa mwaka 1991, alitumia fursa ya kuuza parachichi kuanza
safari yake ya ujasiriamali.
“Baada
ya kukaa nyumbani mwaka mzima bila kazi, ndipo nikaamua kuuza parachichi ambapo
nilikuwa nikizisafirisha kutoka Tarime kwenda kuziuza jijini Mwanza,” anasema Bilali
katika mahojiano maalumu na Mara Onlne
news ofisini kwake, wiki iliyopita.
Tarime
ni miongoni mwa maeneo ya mkoa wa Mara yanayozalisha parachichi kwa wingi. Hivyo,
Bilali alitumia fursa hiyo kupata mtaji na kuingia rasmi katika sekta ya mapambo.
Kutokana
na ubora wa kazi zake, Bilalia ameanza kupata kazi za kupamba sherehe mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
“Hivi
sasa ninapata wateja wa kupambiwa sherehe mbalimbali katika maeneo tofauti ya
Tarime na nchi jirani ya Kenya. Hata hivi karibuni sisi VeeMoney tulipata kazi ya
kupamba jijini Nairobi, Kenya,” anaeleza.
Bilali
anafafanua zaidi kwamba alilazimika kuanza kazi ya ujasiriamali akiwa mwanafunzi
baada ya baba yake kupata ajali iliyomsababisha kushindwa kugharimia mahitajii ya masomo yake.
“Nilianza
kuuza nguo na cheni, nikafanikiwa kupata pesa ya kulipa karo ya mwaka mzima.
Ninamshukuru Mungu kuwa hali hiyo ilinifanya kupenda kazi ya ujasiriamali
badala ya kuajiriwa,“ anasema Bialali.
Kujiamini
kwa Bilali kumemsukuma kujiita Malkia wa Nguvu baada ya kuamini kuwa anaweza
kukabiliana na changamoto za maisha na kusonga mbele kama mwanamke.
Mbali
ya shughuli za mapambo, Bilali anafanya biashara ya kuuza nguo za kisasa na vinywaji
mbalimbali.
Ndoto yake kubwa
Bilali
anasema ndoto yake kubwa ni kuwa mwanamitindo bora ndani na nje ya Tanzania
siku za usoni.
“Ukiangalia
mavazi yangu ni ya kimitindo, lakini moja ya ndoto yangu ni kuwa designer (mwanamitindo)
maarufu na kutoa pia fursa nyingi za ajira kwa vijana wa kike,“ anasema Bilali.
Ujumbe
wa Bilali kwa wanawake wa wilayani Tarime ni kuthubutu kuwa wajasiriamali kwa
kutumia fursa zilizopo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Lakini
pia sisi kama wanawake tunapaswa kupendana na kufanya kazi kwa ushirikiano na
kuondokana na dhana ya utegemezi,” anasema Bilali kuhitimisha mahojiano haya.
No comments:
Post a Comment