NEWS

Saturday 9 May 2020

Musoma Vijijini hakuna kulala ujenzi wa shule


UJENZI wa Shule ya Msingi Butata katika jimbo la Musoma Vijijini, unaendelea kushika kasi kutokana na michango mbalimbali ya wananchi, viongozi wa kijiji, kata, jimbo, serikali na wadau wa maendeleo.

Maktaba moja, vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu vinajengwa kwa wakati mmoja katika shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Butata katani Bukima.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Butata, William Kugosora, ameiambia Mara Online News leo Jumamosi Mei 9, 2020 kwamba katika ujenzi huo, wanakijiji wanachangia nguvukazi ya kusomba mchanga, mawe, kokoto na maji, lakini pia Sh 4,000 kutoka kila kaya.

Kugosora ameongeza kuwa Diwani wa Bukima, January Simula, amechangia saruji mifuko mitano na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amechangia saruji mifuko 100.

“Maktaba ya shule hii ikikamilika, mbunge huyo ataiongezea vitabu vingine,”
 amesema mwenyekiti huyo wa serikali ya kijiji.

Aidha, Shirika la PCI limethibitisha ahadi ya kukamilisha maktaba hiyo kwa kuezeka jengo, ukamilishaji wa ndani na nje pamoja na kuweka samani husika.

Wadau wengine wa maendeleo wanaochengia ujezi wa shule hiyo ni Samson Masawa (USA) na Muya Essero, ambao ni wazawa wa kijiji cha Butata.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Butata, Yohani Dawi, amesema fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu pia zimechangia kugharimia ujenzi huo na kwamba Halmashauri ya Wilaya nayo inakusudia kuchangia.

Diwani wa Bukima, Simula, amewashukuru wakazi wa kijiji cha Butata kwa ari ya ujenzi wa miradi ya maktaba, vyumba vipya vya madarasa na ofisi ya walimu katika shule mpya, zahanati na ofisi ya kijiji hicho.
 
Wananchi katika kijiji cha Butata wakiendelea na ujenzi wa maktaba ya Shule ya Msingi Buatata

Pia ameishukuru Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini kwa kuendelea kuchangia uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika kata ya Bukima inayoundwa na vijiji vitatu; ambavyo ni Butata, Kastamu na Bukima.


Simula amewataja wadau wengine wa maendeleo katika sekta ya elimu katani Bukima kuwa ni PCI, USA ambao wamechangia vitabu, ujenzi wa vyoo, matenki ya maji, kilimo cha mazao ya chakula kwa ajili ya wanafunzi na mafunzo mbalimbali.

Wadau wengine ni BMZ, Ujerumani ambao wamechangia vifaa vya elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu. Pia baadhi ya wazawa wa kata ya Bukima wamekuwa wakijitokeza kuchangia maendeleo katani humo.

Diwani Simula amesema Mbunge Muhongo ameshapeleka michango mingi ya elimu katani humo ikiwemo saruji, mabati, madawati kwa shule za msingi na vitabu kwa ajili ya maktaba za shule za msingi na sekondari.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Muhongo, amesema mfuko wa jimbo nao umechangia saruji na mabati katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu katani Bukima.

(Habari na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages