NEWS

Saturday 9 May 2020

Rais Magufuli amwaga pikipiki kwa maofisa tarafaMAOFISA tarafa mkoani Simiyu wamekabidhiwa pikipiki zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuwanunulia maofisa tarafa wote nchini vyombo hivyo vya usafiri alipokutana nao kwenye kikao kazi jijinima Dar es Salaam, Mei 2019.

Akiwakabidhi pikipiki hizo Ijumaa Mei 8, 2020, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, amewataka maofisa hao kuzitumia kuwafikia wananchi kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Miongoni mwa mambo mengine, Sagini amewaagiza maofisa tarafa mkoani humo kufuatilia kwa karibu mkakati wa elimu kwa njia ya mtandao uliozindulia Mei 4, 2020 kwa ajili ya wanafunzi kipindi hiki cha mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona au COVID-19.

Aidha, Sagini amewataka maafisa tarafa hao kuzitumia pikipiki hizi kwa kuwafikia wananchi wote wakiwemo wakulima hasa kipindi hiki cha mavuno na lengo kuu liwe kuwakumbusha kutouza chakula chote bila kubakiza akiba.
"Tumevuna sana mwaka huu, wito wangu kwenu pikipiki hizi mzitumie kuwafikia wananchi hususan wakulima, wambieni wasiuze chakula chote, wakumbuke kuweka akiba na kidogo watakachouza wakumbuke kukata bima," amesema Sagini na kuongeza:

"Kwenu ninyi maafisa tarafa pikipiki hizi mzitumie kwa malengo kusudiwa, si mtu anachukua chombo hiki anaenda kunywa pombe akirudi amelewa anadondoka nayo, tusingependa kuona vifaa hivi vinaharibiwa kizembe."
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, akimkabidhi Ofisa Tarafa ya Busega, David Pallangyo, kofia na ufunguo ikiwa ni ishara ya kumkabidhi pikipiki.

Awali, Katibu Tawala Msaidizi, Ekwabi Mujungu, amewataka maofisa tarafa hao kutumia pikipiki hizo kuhamasisha shughuli za maendeleo ya jamii ikiwemo kusimamia miradi ya elimu, afya, kilimo na hifadhi ya mazingira.

Aidha, Mujungu ametoa maelekezo kwa makatibu tawala wa wilaya mkoani Simiyu kutenga fedha kwa ajili ya mafuta na matengenezo ya pikipiki hizo ili zidumu muda mrefu.

Akizungumza kwa niaba ya maofisa tarafa mara baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo, Ofisa Tarafa ya Dutwa,   Isabela Nyaulingo, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia usafiri huo akisema vitawarahisishia utendaji kazi na kuahidi kuzitunza vizuri.

Pikipiki 15 zenye thamani ya Sh 33,285,000 zimekabidhiwa kwa maofisa tarafa mkoani humo, ikielezwa kuwa kila moja umegharimu Sh milioni 2,219,000.

maofisa tarafa waliopewa pikipiki hizo ni kutoka tarafa za Dutwa, Nkololo na Muhango (wilayani Baradi), Kivuko na Busega (Busega), Itilima, Kanadi, Bumela na Kinang'weli (Itilima), Mwagala, Sengerema na Nung'hu ( Maswa), Kisesa, Nyalanja na Kimali (Meatu).

(Habari na Anita Balingilaki, Simiyu)


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages