SERIKALI wilayani Bariadi
katika mkoa wa Simiyu, imejipanga kuanza operesheni ya kuwasaka wafanyabiashara
wanaouza sukari kwa bei ya juu, kinyume cha bei elekezi iliyotangazwa na
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara.
Hatua hiyo imetangazwa na
Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga, wakati akizungumza na wafanyabiashara mjini
Bariadi, Ijumaa Mei 8, 2020.
Kiswaga amewataka
wafanyabiashara kuuza sukari kwa bei elekezi ya Sh 2,900 kwa kilo moja na
kuweka bayana kuwa operesheni ya kuwasaka wanaokaidi bei hiyo itaanza rasmi Mei
12, 2020.
“Ni dhahiri kwamba
asilimia kubwa ya wafanyabiashara wameshindwa kufuata maagizo ya serikali ya
kuuza sukari kwa bei ya shilingi 2,900, hivyo kuanzia Jumanne ya tarehe 12 mwezi
huu tutafanya operesheni kali kwenye maduka yote na tutakaokuta wamekiuka
tutawachukulia hatua za kisheria," amesema Kiswaga na kuelezea kukerwa
kwake na upandishaji bei ya sukari kipindi hiki cha mfungo wa Mwenzi Mtukufu wa
Ramadhan.
Kwa upande wake, Katibu wa Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu, Zebedayo Kingi, amesema wengi wanatumia gharama kubwa kufikisha bidhaa zao mkoani humo hali inayowalazimu kuuza kwa bei ya juu zaidi ya bei elekezi.
Hata hivyo, Kingi amesema
wafanyabiashara wa mkoani humo hawana budi kufuata maelekezo ya serikali kwa
kuuza sukari kwa bei elekezi ili kuwezesha wananchi wote kumudu ununuzi wa
bidhaa hiyo.
Naye mfanyabiashara, Bahati
Ntelemko, amesema tatizo la upandishaji bei ya sukari huenda limetokana na
kupungua kwa uzalishaji viwandani, huku akionesha wasiwasi wa hatari ya
kukosekana kwa bidhaa hiyo, hasa maeneo ya vijijini.
(Hanari na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment