NEWS

Friday 8 May 2020

Simanzi: Serengeti yaondokewa kinara wa maendeleo


 DIWANI wa Kata ya Mbalibali wilayani Serengeti, John Ng’oina (CCM), amefariki dunia Alhamisi Mei 7, 2020 nyumbani kwake mjini Mugumu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Juma Hamsini, amezungumza na Mara Online News leo Ijumaa Mei 8, 2020 asubuhi na kuthibitisha kifo hicho.

“Huyu mzee bwana amefariki jana [Alhamisi] nyumbani kwake usiku na tunaendelea kuwasiliana na familia kuhusu namna bora ya mazishi ili kumpuzisha maana ni mtu wa watu, sio tu kutoka Serengeti bali ndani na nje ya Tanzania,” amesema Mhandisi Hamsini.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Ng’oina amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kwa miaka kadhaa sasa na amekuwa akipata matitabu nchini India mara kwa mara.

Ng’oina amekuwa kada mkongwe wa CCM, ambaye amepata kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Serengeti kwa miaka mingi na alitumia nafasi hiyo kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za elimu na afya.
 John Ng'oina akiendesha kikao cha madiwani enzi za uhai wake

                                                         
 “Huyu mzee amekuwa mwenyeki wa halmashauri kwa awamu nyingi na diwani kwa miaka zaidi ya 20. Alikuwa kiongozi wa maendeleo hata kule nyumbani kwao alianzisha Shule ya Sekondari ya Machochwe,” amesema Hamsini.

Ng’oina atakumbukwa pia kwa juhudi zake za kuanzisha ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ya Serengeti ambayo sasa imeanza kutoa huduma kwa wananchi baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kutoa Sh milioni 800 kugharimia ukamislishaji wa baadhi ya majengo muhimu ya hospitali hiyo.

Aidha, Ng’oina alikuwa mmoja wa viongozi waliopigia debe ujenzi wa uwanja wa ndege Mugumu ambao maandalizi yake yamefikia hatua nzuri.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages