NEWS

Saturday 9 May 2020

World Vision yaimwagia Simiyu msaada wa mamilioni kujikinga na Corona


Mkoa wa Simiyu umekabidhiwa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na virusi vya corona ambavyo vitatumika kwenye vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa watakaobainika kuwa na virusi hivyo.

Mbali na vifaa hivyo pia umekabidhiwa zahanati sambamba na vifaa vya matibabu vitakavyotumika kwenye zahanati hiyo ya wigelekelo ambapo makabidhiano hayo yamefanyika jana kwenye Kijiji cha Wigelekelo  eneo ilipojengwa zahanati hiyo wilayani Maswa mkoani hapo.

Awali akikabidhi zahanati na vifaa hivyo meneja wa World Vision Tanzania kanda ya ziwa John Massenza amesema zahanati na vifaa vyote kwa pamoja vimegharamu kiasi cha shilingi milioni 95,755,000.

"Leo tunakabidhi mipira ya kuvaa mikononi boksi 500,vitakasa mikono lita 200,vipaza sauti 26 kwa wahudumu wa afya ngazi za jamii na mavazi  ya kujikinga na maambukizi 60 na barakoa aina ya N95"alisema Massenza.


Aidha aliongeza kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa na waganga wakuu wa wilaya zilizopo mkoani hapo shirika litaendelea kutoa misaada ya vifaa , vitendea kazi, kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na kuhakikisha wanasambaza elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu .

" Shirika limeendelea kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya mapafu  kwa njia ya matangazo na tumewezesha mafunzo kwenye makundi tofauti ya watu ambayo yatasambaza elimu hii kwa jamii mfano wa makundi hayo ni viongozi wa dini,wahudumu wa afya ,viongozi wa  serikali "alisema Massenza.

Mbali na hayo ameishukuru serikali kwa bidii inazozionesha katika kupambana na ugonjwa huo na ushirikiano uliopo baina ya shirika hilo na serikali hatua itakayowezesha kulipunguza na hatimaye kulimaliza tatizo hilo.

Akipokea vifaa hivyo pamoja na zahanati katibu tawala mkoa wa Simiyu Jumanne Sagini amesema kuwa world vision Tanzania wamekuwa waungwana kwani pamoja na kuwa  wanafanya kazi na halmashauri mbili tu  mkoani hapo lakini vifaa walivyotoa  wamevielekeza kwenye halmashauri zote sita za mkoani hapo pasipo ubaguzi.


Nae mganga mkuu wa mkoa wa Simiyu Festo Dugange alisema wamekuwa wakitekeleza hatua mbalimbali za kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo huku akiongeza kuwa mkoa upo vizuri na tayari vimetengwa vituo endapo watapatikana washukiwa wa ugonjwa huo  waweze kutibiwa. 

Akiongea kwa niaba ya wakurugenzi wa halmashauri zilizopo  mkoani hapo mkurugenzi mtendaji wa  halmashauri ya wilaya ya Maswa Dkt Frederick Sagamiko amelishukuru shirika hilo kwa kuwa msaada mkubwa kwenye shughuli za kimaendeleo mkoani hapo hususan kwenye wilaya mbili ambazo linafanyanazo  kazi mkoani hapo ikiwemo Maswa ambapo mbali na kuwajengea zahanati pia wamewajengea kiwanda cha viazi lishe na wilaya ya Itilima kiwanda cha sabuni.

Kwa upande wao wananchi akiwemo Mbuke Kemakema na Mashauri Ngeme wamelipongeza shirika hilo kwa ujenzi wa zahanati kwani awali walitembea umbali mrefu kufata huduma hiyo.

(Habari na Na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages