NEWS

Thursday 9 July 2020

DC Bariadi aonya machinga wanaonyonya wakulima wa pamba

MKUU wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, amesema hatasita kuwachukulia hatua watendaji wa vijiji na mitaa ambao hawatatoa taarifa juu ya machinga wanaonunua pamba ya wakulima kinyume na utaratibu uliowekwa na serikali.
Kiswaga ameyasema hayo jana Julai 9, 2020 wakati akizungumza na watendaji wa serikali, viongozi na wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika na Masoko (AMCOS) cha Nkong'wa kilichopo kata Nkololo na kuongeza kuwa hatakubaliana na machinga wanaowanyonya wakulima kwa kununua pamba yao kwa bei isiyo elekezi na pasipo kufuata utaratibu.

Amesema kitendo hicho kinawaumiza wakulima na kuwasababisha kutopata tija kwenye kilimo na kuongeza kuwa kama alivyofanya msimu uliopita kwa kutaifisha pamba ya magendo iliyokuwa inanunuliwa kwa wizi  utaratibu huo utaendelea na fedha itakayopatikana itatumika kwenye shughuli za kimaendeleo.

"Zipo taarifa juu ya machinga wanaonunua pamba kwa magendo kwa bei ya shilingi 500, 400, 300 mpaka 200, bei ambayo ni ya kinyonyaji... bei elekezi ni shilingi 810, wapo wanaonunua bila kufuata utaratibu wa kununulia kwenye vyama vya msingi vya ushirika, hivyo endapo tutakamata pamba tutaitaifisha na mtendaji, pamba ya magendo ikipatikana kwako na wewe hukutoa taarifa, tutakuchukulia hatua kwani hatutakubaliana na vitendo vya kinyonyaji kwa wakulima," amesema Kiswaga na kuongeza:
Viongozi wa AMCOS ya Nkong'wa na wakulima kikaoni

"Kuhusu wafanyabiashara wenye tabia ya kuwanyonya wakulima, niwatake kuacha mara moja... pamba yote inunuliwe kupitia AMCOS na wafanyabiashara wote wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa na serikali."

Mapema, Afisa Ushirika Wilaya ya Bariadi, Lucas Kiondere, amesema AMCOS 53 wilayani humo zitafanya kazi msimu huu wa 2020/2021 na kwamba wanaendelea na utaratibu wa kubadilisha makatibu wa vyama hivyo wasiokuwa na elimu ya kuanzia kidato cha nne na kuendelea.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima, mzee Charles Nkenyenge amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni kuishi mbali na taasisi za kifedha, hivyo kuomba wasaidiwe kuogezewa huduma, hususan maeneo ya vijijini kwani wanatumia gharama nyingi ikiwemo usafiri kwa ajili ya kufuata hela zao benki.

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages