NEWS

Saturday 11 July 2020

DPP Biswalo awasimamisha kazi mawakili waliofuta kesi ya mauaji ya ajuza Simiyu


MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, amewasimamisha kazi mawakili wawili wa serikali wa mkoa wa Simiyu kwa tuhuma za kuwaachia huru watuhumiwa saba wa mauaji ya ajuza mkazi wa kijiji cha Kinamwigulu wilayani Maswa.

Aidha, DPP Mganga amemwagiza  Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka kuwachukulia hatua za kinidhamu mawakili hao na kuelekeza wasijishughulishe na majalada ya jinai.

DPP Mganga amewambia waandishi wa habari jana Julai 10, 2020 Simiyu kwamba mawakili hao walifuta kesi ya mauaji namba moja ya mwaka 2019.

Amefafanua kuwa kesi hiyo ikikuwa ya mauaji ya ajuza Nchambi Singing’hi na kwamba ufuatiliaji wa ofisi take umebaini kuwa Desemba 23, 2019 watuhumiwa wawili walifutiwa kesi na wakili Twahabu Yahaya na watano walifutiwa kesi ya mauaji Juni 17, 2020 na wakili  Amani Kirua na ufutaji huo haukuandikwa popote sababu za kufuta na hakuna kumbukumbu za kimaandishi kwenye majalada sambamba na uwepo wa vitendo vya rushwa katika kesi hiyo.

                                                    DPP Biswalo Mganga(kulia)na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Miriam Mmbaga


Katika hatua nyingine, DPP Mganga amelitaka jeshi la polisi mkoani Simiyu kuwasaka waliofutiwa mashtaka huku akidokeza kuwa tayari jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wawili ambao hakuwataja majina kwa sababu za kiupelelezi na kwamba watafikishwa mahakamani Jumatatu Julai 13, 2020 kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Miriam Mmbaga, ameahidi kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashikata katika  kukomesha vitendo vya uhalifu kwa jumla mkoani humo.


(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages