KAMA sio mamlaka za
serikali na wasaidizi wa kisheria, mwanafunzi Sikujua Masunga (sio jina lake
halisi) ambaye ni mkazi wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, angekuwa ameolewa, yaani
angekuwa mke wa mtu kwa sasa.
Sikujua mwenye umri wa
miaka 17, alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu (2020) katika
Shule ya Sekondari ya Mwagi wilayani Kwimba. Hata hivyo, mpaka sasa (Julai
2020) hajaripoti shuleni kutokana na kile kinachodaiwa kuwa kuna mkakati wa kutaka
kumuoza.
Inaelezwa kwamba Sikujua
amechumbiwa na mwanaume mkazi mkazi wa mkoani Geita na kinachofanyika sasa ni
maandalizi ya kumtorosha kutoka Kwimba.
Baada ya kupata taarifa
hizo, Mara Online News imefuatilia sintofahamu inayojaribu kumnyima Sikujua haki
yake ya kupata elimu. Mtoto huyo anaishi na mzazi mmoja ambayeni mama yake.
Mara online News
imefanikiwa kufika nyumbani kwao Sikujua, ingawa hata hivyo, haikumkuta
mwanafunzi huyo wala mzazi wake, isipokuwa dada yake aliyejitambulisha kwa jina
la Edna, ambaye amekiri kwamba mdogo wake huyo hajaripoti shuleni kwa ajili ya
kuanza masomo ya kidato cha kwanza.
“Sijui kwanini hataki
kwenda shule, nilimuuliza akasema hataki shule, mama alipotaka kumnunulia uniform
[sare za shule] alikataa akasema hataweza masomo na kwamba mzazi akimlazimisha kusoma
atapoteza hela bure,” amesema dada huyo wa Sikujua.
Taarifa ambazo
hazijathibitishwa zinaeleza kuwa Shene ambaye ni mama mzazi wa Sikujua,
anashirikiana na familia ya mwanaume anayetaka kumuoa mwanafunzi huyo
kumkatisha tamaa ya kusoma.
Njama hizo ziligunduliwa
na watetezi wa kisheria wilayani Kwimba, ambao waliliarifu Jeshi la Polisi
likaenda kuweka shinikizo kwa mzazi wa Sikujua kuhakikisha kuwa mwanafunzi huyo
anaripoti shuleni haraka iwezekanavyo ili kuanza masomo ya kidato cha kwanza.
“Huyo binti mzazi na ndugu
zake walimbana asiende shule ili wamuoze kisirisiri, lakini baada ya kuripoti
taarifa hizo polisi walikwenda wakamuonya mama yake, lakini cha kushangaza
mpaka mwezi huu wa Julai mtoto huyo hajaripoti shuleni,” amesema Mkurugenzi wa
Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani katika mazungumzo na
Mara Online News wilayani Kwimba, juzi.
Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayuko pichani) wilayani humo, juzi. |
Naye Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Luzela, Musa Malole, ameelezea kushangazwa kwake na taswira ya
msichana huyo kutokwenda shule licha ya kumhimiza na mama yake mara kadhaa
kuhusu suala hilo.
“Binti huyu yupo tu
nyumbani, sijafahamu kama ameolewa, nimekuwa nikimhimiza aende shule lakini
haendi,” amesema Malole na kuongeza kuwa anaendelea kushirikiana na mamlaka za
serikali kuhakikisha kuwa mtoto huyo anaendelea na masomo yake.
Kwa mujibu wa Afisa
Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Boresha (Boresha Projecti) Wilaya ya
Kwimba, Respectson Akyoo, mazingira hayo yanayomzunguka Sikujua yanaweza kuwa ukatili
wa kingono unaotishia kumnyima msichana huyo haki yake ya msingi ya kupata
elimu, lakini pia unaoweza kumfanya ashindwe kufikia ndoto yake.
Akyoo amesema ukatili wa
kingono kwa watoto unachangiwa na uelewa duni wa wananchi kuhusu madhara ya
vitendo hivyo, mila na desturi zisizozingatia usalama wa mtoto hali ambayo pia
huchangia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika jamii.
Mradi wa Boresha unatekelezwa
chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania (The Tanzania Interfaith Partnership Association - TIP). Unaoundwa na
taasisi nne za kidini ambazo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la
Kitaifa la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania
(TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).
Maono ya TIP ni
kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania
yenye afya na kizazi kisicho na Ukimwii.
Mkurugenzi wa
Watetezi wa Kisheria, Malole na Mchungaji
Mathias Mleka wa AICT Ngudu, Kwimba wanasema TIP imewapatia mafunzo ambayo
yanawasaidia kuelimisha wananchi madhara ya vitendo vya ukatili ukiwamo wa
kingono kwa watoto katika jamii.
“Tumegundua kwamba watoto
wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono katika sherehe na michezo ya ngoma…
tunashukuru mafunzo tuliyopewa na TIP tunaendelea kuyasambaza na mwitikio wa
jamii ni mkubwa,” amesema Mchungaji Mleka.
Kumekuwepo na juhudi
mbalimbali za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto nchini
Tanzania zikiwamo zinazofanywa na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa
Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Mpango huo wa miaka
mitano, ulianza kutekelezwa mwaka 2017/18 na utafikia kikomo mwaka 2021/22
chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Kwa mujibu wa mchumi
kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Happiness Mugyabuso, mpango huo unalenga
kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2021 ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini
uwe umepungua kwa asilimia 50.
(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Kwimba)
No comments:
Post a Comment