NEWS

Friday 31 July 2020

Changamoto za PF3 zinavyokwaza haki za wahanga wa ukatili Kwimba



PAMOJA na umuhimu wa Fomu Namba Tatu ya Polisi (PF3) katika kumsaidia mhanga hasa wakati wa kutoa ushahidi mahakamani, uelewa, upatikanaji na ujazaji wa fomu hiyo bado ni tatizo linalohitaji ufumbuzi katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Utafiti uliofanywa na Mara Online News katika wilaya hiyo hivi karibuni umebaini kuwa wananchi wengi wakiwamo viongozi hawajui PF3, kazi yake, wala inakopatikana.

Mkazi wa kijiji cha Mwaging’hi, Edna Didas alipoulizwa iwapo anafahamu fomu hiyo amesema “Sijui PF3. Kwani inapatikana wapi, kazi yake ni nini? Naomba unisaidie niijue.”

Mwanamke huyo amesema ni mara ya kwanza kusikia kwamba kuna kitu kinachoitwa PF3 na kusisitiza kuwa hajapata kuona mtu akiwa na fomu hiyo, wala kusikia ikiongelewa na yeyote kijijini hapo.

Mkazi wa kitongoji cha Manguluma, Mchungaji Melkisadick John naye amesema hafahamu PF3 na kazi yake. “Sijui hiyo PF3, sijui kabisa hiyo inahusiana na nini,” amesisitiza huku akishindwa kuitamka kwa usahihi fomu hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luzela, Musa Malole, amesema “Sifahamu PF3, sijui, lakini sikui nimewahi kusikiasikia kitu kama hicho, hapana, niwe mkweli, sijui kabisa.”

Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani na Mratibu wa Ukimwi wilayani humo, Dkt Ally Sadick, wamekiri kuwa PF3 na matumizi yake havifahamiki kwa wananchi wengi.

“Hata upatikanaji wa PF3 bado ni shida wilayani hapa,” amesema Sagalani huku akitolea mfano kesi za wasichana watano waliofanyiwa ukatili wa kingongo zilizoripotiwa ofisini kwake kati ya Mei na Juni mwaka huu akisema kati ya hao, wawili ndio walipata fomu hiyo kwa ajili ya matibabu na ushahidi mahakamani.

Kwa upande wake, Dkt Sadick amesema huduma ya PF3 wilayani Kwimba inakabiliwa na changamoto lukuki zinazohitaji utatuzi ili kuwezesha wahanga wa vitendo vya ukatili kuwa na ushahidi wa kutosha kutetea haki zao mahakamani.

“Kwenye suala la PF3 kuna changamoto nyingi, kwanza sio vituo vyote vina wataalamu wa kuijaza, wengi wanaijaza wanavyoweza, hivyo inakuwa haina ubora unaotakiwa.

“Changamoto nyingine iko kwenye vituo vya afya, anayepaswa kuijaza ni daktari aliyemwona mhanga siku ya kwanza,” amesema Dkt Sadick.

Tafsiri ya maneno hayo ya Dkt Sadick ni kwamba mhanga asipomkuta daktari hukosa huduma ya kujaziwa PF3 na zinazojazwa kwa uelewa binafsi mtu zinakuwa na upungufu wa vigezo muhimu vinavyokubalika kwa ushahidi mahakamani.

Katika kutatua tatizo la uelewa mdogo wa kujaza PF3, daktari huyo ameshauri vyuo husika kuwa na somo maalumu la ujazaji wa fomu hiyo. “Ni vizuri kwenye vyuo vyetu kuwepo na topic (kipengele) maalumu ya kujaza PF3,” amesema.

Dkt Sadick amesema kuwa kwa kufanya hivyo, watapatikana wataalamu wa kujaza PF3 kikamilifu na kwa usahihi, hivyo kuwezesha wahanga kupata msaada unaostahiki kwa upande wa fomu hiyo.

Lakini pia, kukosekana kwa kituo maalumu (One Stop Centre) cha huduma za polisi, matibabu na ustawi wa jamii kwa wahanga wa ukatili, kunatajwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya kukabiliana na vitendo hivyo wilayani Kwimba.

“Huduma hizi zinapokuwa maeneo tofauti wakati mwingine huwakatisha tamaa wahanga kwa kuona watapata usumbufu na kuingia gharama kubwa kuzitafuta," amefafanua.

Hata hivyo, Dkt Sadick na wadau wengine wameshukuru kupata mafunzo ya kupambana na ukatili ukiwamo wa kingono kwa watoto yanayowezeshwa na Mradi wa Boresha unaotekelezwa chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania (The Tanzania Interfaith Partnership Association - TIP).

Ushirikiano huo unaundwa na taasisi nne za kidini ambazo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).

Mchungaji Mathias Mleka wa AICT Ngudu, Kwimba amesema mafunzo hayo yanawasaidia kuelimisha wananchi madhara ya vitendo vya ukatili ukiwamo wa kingono kwa watoto katika jamii.

“Tumegundua kwamba watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono katika sherehe na michezo ya ngoma… tunashukuru mafunzo tuliyopewa na TIP tunaendelea kuyasambaza na mwitikio wa jamii ni mkubwa,” amesema Mchungaji Mleka.
Mchungaji Mathias Mleka wa AICT Ngudu, Kwimba akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani) mjini Ngudu, hivi karibuni

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini, Respectson Akyoo na Afisa Mradi wa Boresha, Hamisi Kibayasi, wamesema ukatili wa kingono unahatarisha haki ya msingi ya elimu kwa mtoto na kumfanya ashindwe kufikia ndoto yake.

Akyoo amesema ukatili wa kingono kwa watoto unachangiwa na uelewa duni wa wananchi kuhusu madhara ya vitendo hivyo, mila na desturi zisizozingatia usalama wa mtoto hali ambayo pia huchangia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika jamii.

Maono ya TIP ni kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania yenye afya na kizazi kisicho na Ukimwii.
Maafisa wa Mradi wa Boresha unaotekelezwa chini ya TIP wakifanya mahojiano na waandishi wa habari mjini Ngudu, Kwimba hivi karibuni.

Kumekuwepo na juhudi mbalimbali za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto nchini Tanzania zikiwamo zinazofanywa na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Mpango huo wa miaka mitano, ulianza kutekelezwa mwaka 2017/18 na utafikia kikomo mwaka 2021/22 chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kwa mujibu wa mchumi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Happiness Mugyabuso, mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2021 ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini uwe umepungua kwa asilimia 50.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Kwimba)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages