Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za ubunge Itilima mkoani Simiyu, jana. |
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, amewataka wakurugenzi watendaji
wa halmashauri nchini kuendelea kuwa wabunifu wa miradi ya kimaendeleo kwenye
halmashauri zao ili kuongeza mapato ya ndani.
Mbali na hilo amewaomba wananchi ambao ni wanachama wa CCM na wa vyama
vingine na wasio na vyama kuwachagua wagombea wa CCM wa nafasi
za urais, ubunge na udiwani ili waende kutekeleza miradi mbalimbali ya
kimaendeleo.
Umati wa wananchi ukimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Itilima, jana.
Majaliwa ameyabainisha hayo jana
wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Itilima, Njalu Silanga (CCM),
ulifanyika kwenye viwanja vya Lagangabilili - itilima mkoani simiyu.
"Itilima ya sasa inapendeza sana ndani ya kipindi cha miaka mitano makao
makuu yanapendeza, yana majengo ya kisasa yenye miundombinu ya kisasa, wananchi
tuchagueni tuendelee kuwaletea maendeleo na tuna mkakati wa kujenga maghala ya
chakula kwenye maeneo yote yanayozalisha chakula kwa wingi," amesema
Waziri Mkuu, Majaliwa.
Aidha, amewataka wananchi kuitunza amani ya nchi hasa tunapoelekea
kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu huku akiwaomba kutumia
haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaoleta maendeleo.
Kwa upande wake, mgombea ubunge jimbo la Itilima, Silanga, amemhakikishia
Waziri Mkuu ushindi wa kishindo kwa wagombea wote wa chama hicho kuanzia nafasi
ya urais, ubunge na udiwani kutokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2015/2020 kwa vitendo na kwa wakati.
"CCM tunaendesha kazi zetu kwa kufuata ilani inasemaje, nami nafuata ilani
inavyosema na hii haina ubishi wana-Itilima ahadi za awamu ya tano zimetekelezwa
kuanzia kwenye sekta ya afya na elimu, wana-Itilima tumetendewa haki, nipeni miaka
mitano tena tuendelee kusogeza maendeleo, ndani ya kipindi changu huwezi kulinganisha
na kipindi kile jimbo lilipokuwa upinzani, siku ya kupiga kura naombeni
mnichaguea mimi niwatumikie," amesema Silanga.
Sehemu nyingine ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge jimbo la Itilima mkoani Simiyu juzi, uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani). |
(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Itilima)
No comments:
Post a Comment