NEWS

Tuesday, 22 September 2020

Tarime waelimishwa mfumo mpya wa ulipaji kodi TRA

Afisa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara, ZAke Rwiza, akielimisha wafanyabiashara mfumo mpya wa ulipaji kodi katika semina iliyofanyika mjini Tarime, leo. (Picha na Peter Hezron)

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imewaelimisha wafanyabiashara katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kuhusu mfumo mpya wa ulipaji kodi za serikali na faida zake kwa watumiaji.

 

Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika mjini Tarime leo Septemba 22, 2020, Afisa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi Mwandamizi wa TRA Mkoa wa Mara, Zake Rwiza, amesema mfumo huo umeanza mwaka huu ambapo ulipaji kodi utakuwa ukifanyika kwa njia ya mtandao tofauti na ilivyokuwa ikifanyika siku za nyuma.

 

Rwiza amesema lengo mabadiliko hayo ni kumrahisishia mteja kulipa kodi akiwa mahali popote, lakini pia kuwezesha serikali kukusanya mapato yake kwa wakati kupitia TRA.

 

Amefafanua kuwa serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020 imefanya mabadiliko kwenye baadhi ya sharia za kodi zinazosimamiwa na TRA ikiwemo Sheria ya Kodi ya Mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani na Sharia ya Madini.

 

Amesema mfanyabiashara anapaswa kuainisha idadi ya wafanyakazi wake na kiasi cha mshahara wanacholipwa ili kuweza kujua kiasi sahihi cha kodi anachopaswa kulipa na kwamba hiyo ni kwa wale wanaolipwa Sh zaidi ya 270,000 kwa mwezi.

 

Rwiza ametaja faida ambazo wafanyabiashara watazipata kutokana na kulipa kodi kwa kutumia mfumo mpya kuwa ni pamoja na wepesi wa kuutumia, kujikadiria wenyewe kiasi cha kulipa kutokana na mapato yao na kulipa ndani ya siku saba tangu akate risiti.

 

Ameongeza kuwa kwa mteja atakayekuwa na sababu ya kumfanya ashindwe kulipa kodi anapaswa kutoa taarifa mapema kwenye mtandao husika ambapo ataelekezwa anachopaswa kufanya na kama amekosea kitu fulani atapiga simu ya huduma kwa wateja na kuhudumiwa bure.

Wafanyabiashara wakimsikiliza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Tarime, Frank Lwesya katika semina ya kuwaelimisha mfumo mpya wa ulipaji kodi, iliyofanyika mjini Tarime leo. (Picha na Peter Hezron)

 

Hata hivyo, Rwiza amesema “Mpaka sasa hivi returns zinazoshughulika na madini, sheli, bima na biashara za ubia hazitalipa kodi kwa njia ya mtandao kwani mfumo wake bado haujakamilika.”

 

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Wilaya ya Tarime, Frank Lwesya, amesema mamlaka hiyo na serikali kwa ujumla inathamini mchango mkubwa wa wafanyabiashara kama wateja wake wa mapato ya fedha yanayotokana na kodi mbalimbali.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Tarime, Frank Lwesya akifafanua jambo katika semina ya kuelimisha wafanyabiashara (hawapo pichani) mfumo mpya wa ulipaji kodi, iliyofanyika mjini Tarime, leo. (Picha na Peter Hezron)


Akizungumza katika semina hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wilaya ya Tarime, Chacha Kisengewa, amempongeza Meneja wa TRA wilayani humo, Lwesya, kwa kazi nzuri anayofanya ikiwemo kusikiliza matatizo ya walipa kodi na kuyatatua.

 

Naye mfanyabiashara Jesca Onyona amesema mfumo mpya wa kulipa kodi kwa njia ya mtandao ni mzuri kwani pamoja na faida nyingine unampatia mfanyabiashara uhuru wa kujikadiria kodi ya kulipa kutokana na faida aliyopata.  

 

(Imeandikwa na Lilian Tesha, Tarime)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages