
Na Mwandishi Wetu
Musoma
----------------
Musoma
----------------
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, amewataka wasimamizi wa elimu katika mkoa huo kutimiza wajibu wao katika ufuatiliaji na usimamizi wa ufundishaji ili kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Akifungua kikao cha majumuisho ya tathmini ya ufaulu wa wanafunzi kwa mwaka 2025 na kuidhinisha mikakati ya mwaka 2026 mjini Musoma hivi karibuni, Kusaya alizitaka halmashauri zote za mkoa wa Mara kuandaa na kutekeleza mikakati ya kuinua ufaulu wa wanafunzi kwa mwaka 2026 katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
“Mkoa wa Mara tunajipanga kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na kuongeza mitihani ya majaribio katika ngazi ya shule, kata, halmashauri na mkoa ili kuwapima wanafunzi na kusahihisha pale tunapoona hatufanyi vizuri kama mkoa kabla ya mtihani wa kitaifa,” alisema.
Kusaya aliwatahadharisha kuwa itafika wakati wasimamizi wa elimu kwa ngazi mbalimbali watawajibishwa kulingana na matokeo ya ufaulu wa wanafunzi, hususan wa shule za msingi na sekondari.
Aliwataka wasimamizi wa elimu ngazi ya mkoa na halmashauri kufanya maboresho katika usimamizi wa elimu na kuongeza ufuatiliaji wa ufundishaji, ujifunzaji madarasani na kuchukua hatua za haraka ili kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, Kusaya aliwataka wasimamizi wa elimu mkoa wa Mara kuimarisha ushirikiano na wadau, hususan wazazi, walezi na viongozi mbalimbali katika jamii ili wasaidie katika kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Awali, akitoa taarifa kwa Katibu Tawala, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu, Dkt. Elpidius Baganda, alisema kikao hicho cha siku moja kina lengo la kufanya majumuisho ya mikakati ya ufaulu iliyopangwa kuanzia ngazi ya shule, kata na halmashauri zote tisa za mkoa wa Mara ili kupata mkakati wa mkoa.
Dkt. Baganda alisema kikao hicho pia kitaandaa ratiba na kuweka mikakati ya matukio yote muhimu ya kielimu kwa mwaka 2026, ikiwemo ufanyikaji wa mitihani ya utayari kwa madarasa yote ya mitihani, mashindano ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA na Wiki ya Elimu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Musoma, Avith Mallya, alimshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa maelekezo aliyoyatoa ili kuinua ufaulu wa wanafunzi katika mkoa huo.
“Sisi kama wasimamizi wakuu wa elimu mkoa wa Mara tunakuahidi tutayafanyia kazi haya maelekezo yote na kuhakikisha tunaboresha kiwango cha taaluma na ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya ndani na ya kitaifa,” alisema Mallya.
Kikao hicho kilihudhuriwa na baadhi ya wataalamu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, maafisa elimu msingi, sekondari, taaluma, takwimu na vifaa, elimu maalum, wadhibiti ubora na maafisa wa TSC kutoka halmashauri zote tisa za mkoa wa Mara, na kilifanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma.
No comments:
Post a Comment