NEWS

Friday 25 September 2020

Kiswaga awataka wajasiriamali kupuuza uzushi dhidi ya vitambulisho vyao

Miongoni mwa wajasiriamali waliotembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga (hayupo pichani) ni hawa wanaojishughulisha na biashara ya samaki wilayani humo.

 

MKUU wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga, amewataka wajasiriamali kupuuza maneno ya uzushi dhidi ya vitambulisho vyao akisema wanaopotosha wameishiwa hoja za kwenye majukwaa.

Kiswaga ameyasema hayo alipofanya ziara na kuzungumza na wajasiriamali katika maeneo tofauti wilayani Bariadi, juzi.


Wajasiriamali wa matunda na mbogamboga nao wametembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga (hayupo pichani).

Baadhi ya wajasiriamali wilayani humo wamesema vitambulisho vinavyotolewa kwa ajili yao vimekuwa msaada mkubwa kwao huku wakiomba viboreshwe kwa kuongezwa jina na picha.

Wamesema kwamba awali kabla ya kupewa vitambulisho walikuwa wakitumia fedha nyingi kulipia ushuru jambo lililosababisha baadhi yao kushindwa kuendesha biashara zao na kuishia kwenye mikopo.

"Vitambulisho hivi vimepunguza mambo mengi, mfano mwanzoni tulitakiwa kulipa ushuru kila siku na gharama kwa mwezi ilikuwa kubwa,” meEsema Ramadhan Kakwamba ambaye ni mchimbaji mdogo wa dhahabu.

"Awali nilikuwa nafuata nyanya kila tenga nalilipia shilingi 1,000 kabla ya kufika mnadani, aliyeniuzia anakatwa, mwenye toroli naye anakatwa, lakini tangu vitambulisho hivi vije mambo ni mazuri, haya makato yote hakuna, tunakuza mitaji yetu hata ambao walikuwa wamekata tamaa ya biashara wamerudi kufanya biashara zao," amesema Martha Mpemba.

Baadhi ya wajasiriamali wilayani Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga (hayupo pichani) alipowatembelea juzi.

Edward Ihoyelo ni daktari anayetoa huduma katika mgodi wa dhahabu wa Burumbaka uliopo kata ya Gasuma wilayani Bariadi, amesema alianzisha duka dogo la dawa akisema vitambulisho vya wajasiriamali vimeondoa kero ambazo wajasiriamali wadogo walikuwa wanakutana nazo na kuongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameongeza ajira kupitia vitambulisho hivyo kwani watu wanajiajiri na kuajiri wengine.


Baadhi ya wajasiriamali wanaouza matunda na mbogamboga wilayani Bariadi, Simiyu wakiwa kazini.

 Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Elias Stephano amesema kwa mwaka 2020 wamepokea vitambulisho 9,000 ambapo awamu ya kwanza walipokea 1,500 na awamu ya pili 7,500 na kwamba mwitikio wa wananchi kuchukua vitambulisho hivyo ni mkubwa na wengi wanasema vimewapunguzia adha ya ushuru wa mara kwa mara.

"Tuna magulio (minada) 21, zamani kila gulio mtu (mfanyabiashara/mjasiriamali) alitozwa shilingi 1,000, ukizidisha kwa mwaka ni pesa nyingi, hivyo ujio wa vitambulisho hivi unawapa nafuu kubwa wananchi,” amesisitiza Stephano.

(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Bariadi)


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages