Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akizungumza na wadau katika mgodi wa dhahabu wa Burumbaka |
SERIKALI imeutaka mgodi wa dhahabu
wa Burumbaka uliopo kata Gasuma wilayani Bariadi, Simiyu kumaliza mgogoro
uliopo la sivyo itaufunga.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alipofanya ziara
mgodini hapo kufuatia mgogoro uliotokea baada ya baadhi ya walioshindwa
kutokubaliana na uongozi mpya.
Kiswaga amesema awali Afisa Madini aliteua kamati ya kusimamia madini isiyo ya
kisheria, hivyo akaleta waraka ambao unataka kuwa na kikundi ambacho kipo
kisheria hatua iliyosababisha kufanya utaratibu wa kupata viongozi kisheria.
"Kuna watu wanapenda vurugu ziendelee ili wajinufaishe wao na kuna
taarifa za utoroshwaji wa madini usiku, tukiwakamata wanaohusika hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao," amesema Kiswaga na kuongeza:
"Hizi virugu hazina afya kwenye uchumi na kama serikali itaona vurugu
zinaendelea tutasimamisha shughuli za mgodi mpaka hapo hali itakapokuwa
vizuri... hatutakubali kuona damu ya mtu inamwagika. Kikubwa hapa kwanza
maslahi ya wananchi hususan wenye mashamba maana awali walikuwa wanalima
hapa na kuvuna."
Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa tayari kuna majina ya watu wanaotajwa
sana yakihusishwa na mgogoro huo, hivyo amemtaka Kaimu Afisa Madini
kuhakikisha watu hao hawakanyagi mgodini hapo.
Mbali na hayo, Kiswaga amesema waliopewa zabuni ni wale ambao
mashamba/makazi yao yamegeuzwa mgodi na ambao ni wazawa, baadaye ikatokea
sintofahamu kutokana na uwepo wa vikundi vilivyopo kwenye mgodi huo kuwa vingi.
"Vikundi vilivyopo ni vingi lakini kikundi cha wenye mashamba ndio
kimetoa mwenyekiti na katibu msaidizi na hapa kinachoonekana kuna
wale walioshindwa ndio wanataka kuhamasisha vurugu," amesema Kiswaga
Sehemu ya eneo la mgodi wa dhahabu wa Burumbaka. |
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Oscar Kalowa amesema
Oktoba 9, 2020 kulikuwa na kikao kilichoitishwa na mamlaka za mkoa kilichofanyika
kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kilichowahusisha wamiliki wa
mashamba na vikundi vilivyoomba zabuni ya usimamizi wa rush (migodi midogo midogo)
ya Burumbaka kwa lengo la kuwakutanisha pamoja wachimbaji ili kufanya
shughuli ya usimamizi.
Mhandisi Kalowa ameongeza kuwa kikao kilikuwa shirikishi na mjadala ulifanyika
kwa mafanikio na vikundi vilivyoshiriki ni kikundi cha wamiliki wa mashamba (Umoja
Burumbaka), ubunifu, Burumbaka Wajasilismali na Umoja ni Nguvu ambapo kwa
pamoja walijadiliana na hatimaye wakaweka uongozi ambao utasimamia Burumbaka
rush.
Awali, baadhi ya wamiliki wa mashamba wamesema hawana imani na uongozi uliowekwa huku wengine wakidai kuwa baadhi ya viongozi waliochaguliwa sio waaminifu.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment