MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Elias Ntiruhungwa ameeleza kushangazwa na vitendo vya wanachama wawili wa Chadema walioenguliwa kugombea udiwani kuendelea kujinadi kwa wananchi katika mikutano ya kampeni.
Ntiruhungwa amewataja wanasiasa hao na kata zao zikiwa kwenye mabano kuwa ni Bashiru Abdallah (Nyamisangura) na Pamba Mwita (Sabasaba).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Oktoba 19, 2020, Ntiruhungwa amesisitiza kuwa kinachofanywa na Abdallah na Mwita ni ukiukwaji mkubwa wa maadili ya uchaguzi na upotoshaji wananchi.
Amefafanua kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitupilia mbali rufaa za wanasiasa hao na kwamba Oktoba 7, 2020 Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Lucas Ngoto na Katibu wa chama hicho Jimbo la Tarime Mjini, Peter Magwi walikabidhiwa kwa maandishi barua za uamuzi huo.
“Walikata rufaa baada ya utuezi wao kuenguliwa, na Tume ilitupilia mbali rufaa zao baada ya kutokidhi vigezo. Sasa wanafanya kampeni za nini?” amehoji Ntiruhungwa.
Kutokana na hali hiyo, msimamizi huyo wa uchaguzi amewataka Abdallah ambaye ni Mkwenyekiti wa Chadema Jimbo la Tarime Mjini na Mwita ambaye ni Katibu Mwenezi wa chama hicho Kata ya Sabasba kuwambia ukweli wananchi kwamba wao sio wagombea tena ili kutovuruga uchaguzi.
“Hao ni viongozi, wanachofanya ni kuleta chuki na uchochezi. Hakuna uchaguzi wa nafasi ya udiwani katika kata hizo mbili. Kama wangerejeshwa siwezi kukatalia barua zao, wawaeleze wananchi ukweli,” amesisitiza msimamizi huyo wa uchaguzi jimbo la Tarime Mjini.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi katika jimbo hilo, Ntiruhungwa amesema yanaendelea vizuri na ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wananchi wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 28, 2020.
“Vituo vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. Natoa wito kwa wananchi wote waliojiorodhesha kwenye daftari la kupiga kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura,” amesema Ntiruhungwa na kuongeza “Maandalizi hadi sasa yamefikia asilimia 85 na bado tunaendelea kupokea vifaa vya uchaguzi kutoka NEC.”
Wakati huo huo, Msimamizi huyo wa uchaguzi jimbo la Tarime Mjini leo amebandika tangazo la uchaguzi, yaani notice of elections katika vituo vyote 181 vilivyotengwa jimboni humo kama sehemu ya kuwaandaa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu.
Tangazo hilo lina taarifa muhimu ikiwemo orodha ya wapigakura wa jimbo hilo. “Sisi tumejipanga vizuri sana na kila mwannchi atapata fursa ya kupiga kura kwa amani,” amesema.
Katika hatua nyingine, Ntiruhungwa amesema wamejipanga kutangaza wagombea watakaoshinda bila vitisho. “Sisi ni maafisa wa Tume, tutatangaza atakayeshinda. Ombi langu ni kila mgombea kutumia fursa iliyobaki vizuri kutoa sera zitakazoshawishi wananchi kumchagua. Waache presha, tutatangaza atakayeshinda,” amesisitiza.
(Habari na picha na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment