NEWS

Sunday 4 October 2020

Orodha ya wagombea kura za maoni CCM wanaochangia kuimarisha kampeni za ubunge Tarime Mjini, Vijijini

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (kushoto) akipokea mchango wa kununua mafuta ya gari kutoka kwa makada wa chama hicho, Peter Bhusene (wa pili kushoto) na Nicodemus Keraryo (wa pili kulia). Kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka. Mchango huo ni kwa ajili ya kuimarisha kampeni za Waitara na Michael Kembaki anayegombea ubunge jimbo la Tarime Mjini.

 

BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliogombea kura za maoni kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika majimbo ya Tarime Mjini na Vijijini, licha ya kutoteuliwa wamekuwa msaada mkubwa kwa makada wenzao walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro hicho.

 

Wanachama wa CCM waliogombea kura za maoni kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini ni 25 ambapo bahati hiyo ilimwangukia Michael Kembaki ambaye sasa ndiye mgombea wa nafasi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

 

Kwa upande wa jimbo la Tarime Vijijini, idadi ya wana-CCM walioshiriki kwenye kura za maoni kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea ubunge wa jimbo hilo ni 30 lakini aliyefanikiwa kupenya katika mchujo huo ni Mwita Waitara.

Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara akijinadi kwa mamia ya wananchi katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika mjini Nyamongo, Alhamisi iliyopita.


Hata hivyo, katika kuthibitisha uzalendo wao kwa CCM, baadhi ya wanachama ambao hawakufanikiwa kuteuliwa kugombea ubunge wamejitokeza kuchangia misaada ya hali na mali kwa ajili ya kuimarisha kampeni za ubunge kwenye majimbo ya Tarime Mjini na Vijijini.

 

Wanachama hao ni Peter Amos Bhusene, Nicodemus Keraryo, CPA Lucas Magoti, Eliakim Maswi, Hezbon Peter Mwera, Dkt Edward Machage, David Nyamhanga, Darius Ngocho, Dkt Veronica Robert, Deo Meck, Suzy Chambiri, Jackson Kangoye, Mwalimu Mwita Jacob Marwa na Joyce Mang’o.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya CCM Wilaya ya Tarime, michango iliyotolewa na inayoendelea kutolewa na wanachama hao ni pamoja na fedha za kununua mafuta, magari ya kutumika kwenye kampeni na ushiriki mpana katika kampeni za ubunge za Kembaki (Tarime Mjini) na Waitara (Tarime Vijijini).

Mgombea Ubunge Jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya CCM, Michael Kembaki akiomba kura kwa umati mkubwa wa wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni jimboni humo, hivi karibuni.


Jana Jumamosi, Bhusene kwa niamba ya makada wenzake waliochanga fedha ya kununua mafuta ya gari lita 500 kwa ajili ya kuimarisha kampeni za wagombea ubunge hao, amekabidhi mchango huo kwa Waitara katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi ya CCM Wilaya ya Tarime, mbele ya Katibu wa Wilaya, Hamis Mkaruka.

 

Bhusene amesema lengo la mchango huo na ushiriki wao kwenye kampeni za wagombea ubunge hao wa CCM ni kupanda mbegu ya uzalendo, lakini pia kung’oa mbegu ya usaliti ndani ya chama hicho na kuweka kumbukumbu ya ushiriki wa wagombea wa kura za maoni katika kuwaunga mkono walioteuliwa na chama kwenye kampeni ili waweze kupata ushindi mnono.

 

“Tunaungana ili kupata ushindi wa Waitara - Tarime Vijijini na Kembaki - Tarime Mjini. Pia mchango huu unapanda mbegu ya uzalendo ndani ya chama chetu cha CCM, lakini pia unalenga kung’oa na kuchoma mbegu ya usaliti ndani ya chama. Tunaomba wenzetu ambao hawajashiriki kabisa kwenye kampeni wafanye hivyo,” amesisitiza Bhusene.

Peter Amos Bhusene ni miongoni mwa wanachama 30 wa CCM waliogombea kura za maoni kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika jimbo la Tarime Vijijini 2020.


Naye kada kijana wa CCM, Keraryo amesema wamejipanga kuendelea kuwasaidia Waitara na Kembaki kwa hali na mali ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi wa mnono katika kinyang’anyiro cha ubunge na kuwezesha wananchi wa majimbo hayo kupata maendeleo ya kweli.

 

“Tarime tumebaki nyuma kimaendeleo muda mrefu, tunahitaji sasa majimbo haya ya Tarime yafanane na utajiri wa rasilimali zilizopo,” amesema Keraryo.

 

Akizungumza baada ya kupokea mchango huo wa mafuta ya gari, Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), amewashukuru makada wa CCM walioutoa akisema wameonesho uzalendo na upendo wa hali ya juu ndani ya chama hicho.

 

“Hii ni dalili njema ya ushindi ambao sio wa Waitara na Kembaki pekee bali ni ushindi wa CCM na wana-Tarime kwa ujumla, wananchi wetu watarajie kupata maendeleo makubwa baada ya ushindi wetu,” amesema Waitara.

 

#Mara Online News-Election2020Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages