NEWS

Thursday 15 October 2020

Waitara aisimamisha kata ya Nyakonga


 
Mamia ya wakazi wa kata  Nyakonga , jimbo la Tarime vijijini wakimpokea  mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM  Mwita Waitara leo Oktoba 15, 2020

Akihutubia mkutano huo uliofanyika kijijini Kebweye, Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tamisemi kwenye Ofisi ya Rais, amesema akipata ridhaa ya kuwa mbunge, atashirikiana na Simion K. Samwel maarufu kwa jina la ‘K’ anayegombea udiwani wa kata hiyo kupitia CCM kupaisha maendeleo ya wana-Nyakonga.

 

Waitara akionekana mwenye furaha, kulia ni mgombea udiwani kata ya Nyakonga kwa tiketi ya CCM Simon K. Samwel'

Pamoja na mambo mengine, Waitara ameahidi kushirikiana na ‘K’ kuhakikisha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vinapata mikopo ya fedha isiyo na riba kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

 

Waitara akiwaomba kura wakazi wa kata Nyakonga leo 

Mgombea ubunge huyo ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi wa kata ya Nyakonga kumchagua Dkt John Magufuli kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili yeye na ‘K’ wapate nguvu ya kumwomba fedha za mikopo hiyo na maendeleo mengine ya kisekta katani humo.

 

Ametaja miradi watakayoanza kutekeleza katika kata ya Nyakonga baada ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwala huu kuwa ni pamoja na kupeleka hudum,a ya umeme na ujenzi wa nyumba ya mganga wa kituo cha afya katika kata hiyo.

Mamia ya wananchi wakisikiliza sera za mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kupitia CCM, Mwita Waitara (hayupo pichani) katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika kijijini Kebweye, leo.

 

Waitara amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli hivi karibuni imepeleka Sh milioni 40 kugharimia uboreshaji wa mradi wa maji katani Nyakonga, achilia mbali mamilioni mengine ya shilingi yaliyoelekezwa kwenye sekta za elimu na barabara.

 

Baada ya Nyakonga, Waitara amehutubia mkutano mkubwa wa kampeni katika kata ya Binagi ambapo ameainisha namna ilivyopendelewa na Rais Magufuli kwa kupewa miradi mingi ya maendeleo ya wananchi.

 

Ametaja upendeleo huo kuwa ni pamoja na Sh milioni 564 zilizopelekwa kugharimia uboreshaji wa kituo cha afya na mamilioni mengine kadhaa yaliyoelekezwa katika uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari za Kibogwe na Nyamwigura.

Kada wa CCM, Mwita Waitara (mwenye kofia ya njano juu) akiomba kura za ubunge wa jimbo la Tarime Vijijini kwa wakazi wa kata ya Binagi katika mkutano wake wa kampeni leo. (Picha zote na Peter Hezron)

 

Katika hatua nyingine, Waitara amemmiminia sifa Marwa Marigiri anayetetea kiti cha udiwani wa kata ya Binagi kupitia CCM akisema amefanya kazi nzuri sana ya kutetea maendeleo ya kisekta kwa ajili ya wananchi wa kata hiyo.

 

Waitara ametumia nafasi hiyo pia kujipongeza kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia shule ya Nyasaricho msaada wa mabati 216 hata kabla ya kuwa mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini.

 

Fedha nyingine zilizotolewa na Rais Magufuli, kwa mujibu wa Waitara, ni Sh milioni 919 kwa ajili ya kulima barabara kutoka kata ya Nkende hadi kijiji cha Magoma kilichopo kata ya Binagi.

 

“Kwa kuwa tumewapendelea sana hapa Binagi, tunatarajia kura nyingi kwa ajili ya Marigiri kuwa diwani, tunatarajia kura nyingi kwa ajili ya mimi Waitara kuwa mbunge [wa Tarime Vijijini] na tunatarajia kura nyingi sana kwa ajili ya Rais Magufuli,” Waitara amewambia wakazi wa kata ya Binagi.

 (Imeandikwa na Christopher Gamaina, Tarime)No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages