NEWS

Thursday 29 October 2020

Waitara, Kembaki wacheka ubunge Tarime, Heche, Matiko wapigwa

Mamia ya wananchi wakishangilia ushindi wa wabunge kupitia CCM wa majimbo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini kwenye ofisi ya chama hicho mjini Tarime leo. 


WAGOMBEA ubunge katika majimbo ya Tarime Mjini na Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameibuka washindi dhidi ya washindani wao kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Vijijini, Apoo Tindwa, leo Oktoba 29, 2020 amemtangaza Mwita Waitara wa CCM kuwa mshindi wa jimbo hilo baada ya kuvuna kura 35,758 dhidi ya John Heche wa Chadema aliyepata kura 18,757 na Charles Mwera wa ACT Wazalendo (kura 941).

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Vijijini, Apoo Tindwa (kushoto) akimkabidhi mbunge mteule wa jimbo hilo, Mwita Waitara (CCM) hati ya ushindi leo.


 

Kwa upande wa udiwani katika jimbo la Tarime Mjini, wagombea kupitia CCM nao wameibuka washindi katika kata 25 kati ya 26 zinazounda jimbo hilo, huku kata moja ikichukuliwa na mgombea kwa tiketi ya Chadema. 


Naye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Elias Ntiruhungwa, amemtangaza Michael Kembaki (CCM) kuwa mshindi wa jimbo hilo baada ya kupata kura 18,235 dhidi ya Esther Matiko wa Chadema (kura 10,873).

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime Mjini, Elias Ntiruhungwa (kushoto) akimkabidhi mbunge mteule wa jimbo hilo, Michael Kembaki (CCM) hati ya ushindi leo.


 

Kuhusu viti vya udiwani, wagombea kwa tiketi ya CCM wameibuka washindi katika kata zote nane zinazounda jimbo la Tarime Mjini.

 

Akizungumza na wananchi katika mji wa Nyamwaga, Tarime Vijijini mara baada ya kutangazwa mshindi, Waitara amesema ahadi zote alizoahidi wakati wa kampeni atahakikisha anazitekeleza na kwa kuyagusa makundi yote ya wananchi.

Mbunge mteule wa jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (wa pili kushoto) akishukuru wananchi baada ya kutangazwa mshindi leo asubuhi. Wa kwanza kushoto ni Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Apoo Tindwa, wa pili kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Wilaya, Malema Solo (kulia).


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho, amewashukuru wananchi wa majimbo hayo kwa kukiamini na kukipatia chama hicho ushindi wa kishindo katika nafasi za urais, ubunge na udiwani. 


(Habari na picha zote na Mara Online News)




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages