NEWS

Monday 23 November 2020

CCM Tarime waahirisha kuchagua wagombea uenyekiti wa halmashauri

Madiwani wateule wakiwa katika kikao hicho cha uchaguzi kilichoahirishwa leo. Kulia ni Diwani mteule wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye (kulia) ambaye ni mmoja wa wawania nafasi ya uenyeki wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara kimeahirisha uchaguzi wa madiwani wateule wanaonia uenyekiti wa halmashauri za Tarime Mjini na Vijijini.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Marwa Ngicho (kulia) akiahirisha kikao kilichokuwa kichague wagombea nafasi ya uenyekiti katika halmashauri za Tarime Mjini na Vijijini leo. Wengine waliokaa kutoka kushoto ni wabunge, Ghatty Chomete (Viti Maalumu Mkoa wa Mara), Michael Kembaki (Tarime Mjini) na Mwita Waitara (Tarime Vijijini).

 

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Marwa Ngicho, ameahirisha uchaguzi huo kwenye ukumbi wa chama hicho mjini Tarime, leo Novemba 23, 2020.

 

Ngicho amesema wameahirisha uchaguzi huo kutekeleza maagizo waliyopata kutoka ngazi ya juu ya chama hicho tawala.

Madiwani wateule wakifuatilia jambo kikaoni kabla ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa wagombea nafasi za uenyekiti wa halmashauri za Tarime Mjini na Vijijini leo.

 

Taarifa zaidi zilizopatikana nje ya ukumbi zinasema uchaguzi huo umeahirishwa kupisha marekebisho ya uteuzi wa madiwani wa viti maalumu katika halmashauri hizo.

 

Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ukiacha madiwani, ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghatty Chomete, Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka na Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa wilaya hiyo, Solo Malema.

Baadhi ya madiwani wateule wanaowania nafasi ya uenyekiti wa halmashauri za Tarime Mjini na Vijijini wakiwa kikaoni kabla ya uchaguzi huo kuahirishwa leo. Kutoka kulia ni Simon K. Samwel kutoka kata ya Nyakonga, Daniel Komote (Nkende), Msety Gotora (Bomani) na John Bosco (Regicheri).

 

Madiwani wateule wanaochuana katika kinyang’anyiro cha nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini ni Godfrey Kegoye kutoka kata ya Matongo, Simon K. Samwel (Nyakonga) na John Bosco (Regicheri).

 

Kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Tarime madiwani wateule wanaochuana ni Daniel Komote (Nkende), Msety Gotora (Bomani) na Daudi Wangwe maarufu kwa jina la Ngamia (Ketare).

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages