NEWS

Tuesday 24 November 2020

Makuruma ang'ara uenyekiti Halmashauri ya Serengeti

Diwani mteule wa Kata ya Busawe, Ayub Makuruma, aliyechaguliwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wamemchagua kwa kishindo Diwani mteule wa Kata ya Busawe, Ayub Makuruma, kugombea nafasi ya uenyekiti wa halmashauri hiyo.

 

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo jioni Novemba 24, 2020 kwenye ukumbi wa CCM Wilaya ya Serengeti, Makuruma amepigiwa kura za ndiyo na wajumbe wote 40, huku Diwani mteule wa Kata ya Issenye, Mosi Nyarobi aliyejiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho dakika chache kabla ya uchaguzi kuanza akikosa kura.

Diwani mteule wa Kata ya Busawe, Ayub Makuruma (kushoto), akiomba kura kwa madiwani wenzake kabla ya kuchaguliwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

 

Kwa upande mwingine, Diwani mteule wa Kata ya Kisangura, Samson Wambura, amechaguliwa kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo baada ya kupata kura 25 dhidi ya Mosi Nyarobi aliyepata kura 15 na Maranya Baruti ambaye hakupata kura.

 

Pia wajumbe wa kikao hicho wamemchagua Diwani mteule Andrea Mapinduzi kugombea nafasi ya Katibu wa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti – kwa kura 20 dhidi ya Jackline Mwita aliyepata kura 17 na Musa Mseti aliyeambulia kura tatu.

Diwani mteule wa Kata ya Busawe, Ayub Makuruma akizungumza baada ya kuchaguliwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti leo.

 

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Makuruma amemshukuru Mungu kwa kuwajaalia uchaguzi mwema na kutangaza kuwa ushindi wake ni wa Serengeti nzima.

 

Aidha, Makuruma ameahidi kushirikiana na madiwani, watumishi wa halmashauri hiyo na Mbunge wa Jimbo la Serengeti katika kubuni na kutekeleza mipango ya maendeleo ya wananchi.

Msimamizi wa uchaguzi, Abubakar Ghati ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mara, akizungumza katika kikao hicho leo.

 

Awali, msimamizi wa uchaguzi huo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara, Abubakar Ghati, aliwataka wajumbe wa kikao hicho kuchagua viongozi bora watakaoshirikiana nao bega kwa bega katika kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho leo. Anayemfuatia ni mgombea uenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mkuruma. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Serengeti, Jeremiah Amsabi.

 

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche, amewataka madiwani hao kuendeleza umoja wao na kutanguliza maslahi ya wananchi katika utendaji kazi wao.

 

Naye Mbunge wa Serengeti, Jeremiah Amsabi, ameahidi ushirikiano wa dhati kwa madiwani hao katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokwaza maendeleo ya wananchi jimboni humo.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages